Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu
Kawawa amewataka wananchi wa vijiji vya Chamakweza na Pingo katika halmashauri
ya Chalinze kuheshimu mipaka ya vijiji vyao na kuacha tabia ya kuuza ardhi
kiholela pasipo kuzingatia sheria taratibu na kanuni za ardhi.
Kawawa ameyasema hayo katika mikutano
ya kusikiliza kero na migogoro ya ardhi kwa wananchi wa vijiji vya Chamakweza
na Pingo ambapo katika mikutano yake hiyo wananchi walitoa malalamiko yao kwa
kueleza kuwa mipaka ya vijiji hivyo ina utata unaosababisha baadhi ya wananchi
kuuza ardhi ya upande wa kijiji jirani bila kujiridhisha kama eneo linalouzwa
liko katika kijiji cha mtu anayeuza hivyo kusababisha mtafaruku baina ya pande
mbili za vijiji jirani.
Mkuu wa wilaya katika kutafuta ukweli
wa malalamiko ya pande zote mbili alifanya mkutano katika kijiji cha Chamakweza
na kusikiliza malalamiko ya wananchi hao ndipo alienda hadi eneo linalosemekana
kuuzwa kiholela, na baada ya hapo alienda moja kwa moja katika kijiji cha Pingo
na kufanya mkutano na wananchi, pia alisikiliza malalamiko yao dhidi ya upande
wa pili.
Kawawa baada ya kupata malalamiko ya
wananchi wa vijiji hivyo alitaka maelezo kutoka ofisi ya ardhi wilaya kuhusu
malalamiko ya wananchi hao kuhusu mpaka wa vijiji hivyo.
Mtaalamu wa upimaji ardhi Jackson
Mchomvu alibainisha mipaka ya vijiji hivyo ambavyo vilipimwa na wataalam wa
wizara ya ardhi tangu mwaka 2010, na musema kuwa, mpaka halisi unaotenganisha
hivi vijiji kutoka kusini hadi kaskazini ni kutoka mto Msua hadi mto Mbiki, ndio
mpaka unaotambulika kwa sasa ambapo awali mto Mbiki ndio uliotenganisha vijiji
vya Talawanda na Chamakweza kwa upande wa Mashariki na Pingo kwa upande wa
Magharibi.
Kwa mujibu wa mtaalam huyo eneo
kutoka Mto Mbiki hadi Mto Mpapaya ni eneo ambalo lilikuwa halijapata muafaka
kuwa ni la upande wa Chamakweza au Pingo.
Mwaka 2014 wataalam kutoka wizara ya
ardhi walifika ili kukaa na wananchi kuhusu eneo ambalo halikupata muafaka
wananchi wa pande zote mbili hawakuweza kukubaliana hivyo muafaka
haukupatikana.
”Kimsingi eneo hili ndiyo chanzo cha
migogoro na mwingiliano wa wananchi katika matumizi ya ardhi hii”. Mchomvu
alisema.
Baada ya ufafanuzi uliotolewa na
Mpima Ardhi wa halmashauri na kupata uhalisia wa mipaka ya kila kijiji, Mkuu wa
wilaya alitoa maagizo kwa wananchi wa vijiji vyote viwili kuheshimu mipaka hiyo
na kuheshimu matumizi ya ardhi kutokana na mpango wa matumizi sahihi ya ardhi, viongozi
kuheshimu sheria ya ardhi kwa kuacha uuzaji wa ardhi ya kijiji kiholela ili
kuepuka migogoro ya ardhi inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Aidha, Kawawa aliendelea kusema, kwa
kipande cha ardhi ambacho bado hakijafikiwa muafaka na vijiji vyote viwili
yaani kutoka mto Mbiki hadi Mpapaya kitapatiwa muafaka na wananchi wa pande
zote mbili.”
Hivyo wananchi wa Chamakweza na Pingo
wataalam wa wizara ya ardhi watafika kuiweka sawa mipaka yenu toeni ushirikiano
kwa wataalam hao ili mufikie makubaliano yenye tija na yenye kutatua migogoro
kwa pande zote mbili.” Mkuu wa wilaya alisisitiza.
No comments:
Post a Comment