By TMA
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kupitia programu ya Huduma za Hali ya Hewa ya kidunia (Global Framework for Climate Services (GFCS)) iliyo chini ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), imekutana na wadau wa sekta mbalimbali ili kujadili na kupata maoni yao jinsi watakavyoutumia utabiri wa msimu wa mvua za vuli (Oktoba hadi Disemba, 2019) unaotarajiwa kutolewa rasmi tarehe 03 Septemba 2019.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO, Dkt. Agnes Kijazi aliwakumbusha washiriki kutambua mabadiliko ya hali ya hewa ni changamoto kubwa katika sekta mbalimbali hivi sasa, hivyo aliwataka washiriki kufanya juhudi za pamoja ili kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zinatumika ipasavyo na kuleta maendeleo endelevu hasa kuchochea uchumi wa viwanda katika Taifa letu kwa kuzalisha malighafi zitakazohitajika viwandani.
“Ni matumaini yangu baada ya kikao hiki TMA kwa kushirikiana na ninyi wadau kutoka katika sekta mbalimbali tutahakikisha watanzania wanapata taarifa za hali ya hewa kwa wakati na wanazitumia ipasavyo katika sekta mbali mbali ili kuleta maendeleo endelevu hasa kuchochea uchumi wa viwanda katika Taifa letu kwa kuzalisha malighafi zitakazohitajika viwandani ikiwemo mali ghafi kutoka sekta ya kilimo”, alifafanua Dkt. Kijazi
Aidha Dkt.Kijazi alisisitiza wadau kupanga mipango ya sekta zao kulingana na utabiri wa hali ya hewa utakaotolewa hapo baadae wenye kujumuisha maoni yao, ikiwa ni moja ya utekelezaji wa maelekezo kutoka Shirika la hali ya hewa Duniani la kutaka taasisi za hali ya hewa kuwahusisha zaidi wadau ambao ndiyo watumiaji wa taarifa za hali ya hewa.
Washiriki wa mkutano huo ulijumuisha sekta ya afya, nishati, maafa, wanahabari, kilimo, uchukuzi, uvuvi, mifugo, NGO, na wataalamu wa lugha (BAKITA).
No comments:
Post a Comment