Tuesday, September 10, 2019

NG'OMBE ELFU KUMI WAVAMIA DUTUMI

Na Omary Mngindo, Mlandizi

Ng'ombe zaidi ya elfu kumi wanadaiwa kuingia katika Kijiji cha Madege kilichopo Kata ya Dutumi wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani pasipokufuata taratibu.

Hali hiyo inasababisha kuleta migogoro kati ya wenye mifugo hiyo na wakulima, ambao ndio wamiliki wa maeneo hayo kutokana na kutengwa maalumu kwa ajili ya kilimo na si kufugia.

Diwani wa Viti Maalumu Tarafa ya Ruvu Ester Dikoko, ameyaeleza hayo nwishoni mwa wiki kwenye baraza la madiwani chini ya Mwenyekiti Mansour Kisebengo, Makamu Fatma Ngozi aliyemaliza muda wake na Mkurugenzi Mtendaji Butamo Ndalahwa.

"Katika maeneo hayo hali ni mbaya, kuna kundi kubwa la mifugo ipatayo zaidi ya elfu kumi imeingia katika Kijiji cha Madege, hali inayosababisha migogoro isiyokwisha kuhusiana na uingiaji kwenye mashamba na kula vyakula," alisema Dikoko.

Nae diwani wa Kata ya Magindu Issa Mkali yeye ameiomba ofisi ya Mkurugenzi kutenga pesa katika bajeti ijayo, kwaajili ya kuboresha eneo la mnada wa mifugo uliopo Kijiji cha Magindu kwakuwa hauna mazingira mazuri.

"Niiombe ofisi ya Mkurugenzi katika bajeti ijayo itenge fedha kwa ajili ya kuboresha eneo la mnada kijiji cha Magindu, kwani kwa sasa una mazingira mabaya, jamii ya wafugaji na watu wanaopeleka biashara tofauti wanalalamikia mazingira yaliyopo," alisema Mkali.

Baada ya taarifa hiyo Kisebengo alimtaka Mwenyekiti wa Kamati husika Mohamed Samara atolee maelezo suala la mifugo, ambapo Samata alisema kuwa mifugo hiyo imeshaondolewa, imeelekea maeneo ya Kibiti na Rufiji.

"Mheshimiwa Mwenyekiti suala la mifugo ni kweli lilikuwepo lakini Kamati ya Ulinzi na Usalama imeshaipatia ufumbuzi kwa kuondolewa, na kwa taarifa iliyopo ni kwamba imeelekea maeneo ya Kibiti na Rufiji," alisema Samata.

Kuhusiana na suala la uboreshaji wa eneo la mnada wa mifugo, Mwenyekiti Kisebengo ameitaka ofisi ya Mkurugenzi kwenda kulifanyia kazi suala hilo, ili kuipatia ufumbuzi.

No comments:

Post a Comment