Friday, September 13, 2019

SERIKALI YATOA ONYO UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wadau watakaoshiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wahakikishe wanajiepusha na vitendo vya rushwa na uvunjifu wa amani kwani Serikali haitasita kuchukua hatua pale itakapothibitika vitendo hivyo kufanyika.

Waziri Mkuu amesema wadau hao mbalimbali kutoka katika Vyama vya Siasa, Taasisi za Serikali na Zisizo za Serikali na wananchi ni vyema wakahakikisha wanasoma na kuelewa kanuni na miongozo ya uchaguzi huo ili waweze kushiriki ipasavyo.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Septemba 13, 2019) , wakati akiahirisha mkutano wa 16 wa Bunge la 11, Bungeni jijini Dodoma. Waziri Mkuu amewataka Watanzania wote wenye sifa washiriki uchaguzi huo kwani ni haki yao ya msingi.

“Natoa wito kwa Watanzania wote wenye sifa wajiandikishe katika orodha ya wapiga kura, wachukue fomu za kugombea nafasi mbalimbali na kushiriki kupiga kura kwani hiyo ni haki yao ya kikatiba kwa kuzingatia misingi ya demokrasia.”

Mbali na wadau hao, pia, Waziri Mkuu amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama vishiriki kikamilifu katika kuhakikisha wananchi wanafanya uchaguzi kwenye mazingira ya amani na utulivu bila kubugudhiwa.

Waziri Mkuu amewataka Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa uchaguzi huo wahakikishe wanazielewa kanuni na miongozo ilitoyotolewa ili waweze kutoa tafsiri sahihi wakati wa kusimamia uchaguzi huo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewahimiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya waratibu vizuri shughuli za uchaguzi kwenye maeneo yao na wahakikishe uwepo wa ulinzi na usalama wakati wote wa uchaguzi hasa kipindi cha kampeni na wakati wa kupiga kura.

Waziri Mkuu amewasihi wabunge na madiwani wawahamasishe wananchi ili watumie haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa. “Natoa rai kwenu mhakikishe mnashiriki kikamilifu katika shughuli zote za uchaguzi huo.”

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika tarehe 24 Novemba 2019. Uchaguzi huo unafanyika kila baada ya miaka mitano kwa lengo la kukidhi matakwa ya Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, inayoelekeza kuwa Mamlaka na Madaraka ya Serikali yanatokana na wananchi.

Kuhusu uboreshaji wa daftari la wapiga kura, Waziri Mkuu amesema tarehe 18 Julai 2019 Serikali ilizindua zoezi hilo mkoani Kilimanjaro na kuongeza kuwa uboreshaji huo, unahusisha wapiga kura waliotimiza umri wa miaka 18 na wale watakaotimiza umri huo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.

“Makundi mengine yatakayohusika ni wapiga kura waliohamia katika kata au jimbo jingine la uchaguzi, waliopoteza kadi au kuharibika, wanaohitaji kurekebisha taarifa zao; mfano majina ambayo hapo awali yalikuwa yamekosewa pamoja na kuwaondoa wapiga kura waliopoteza sifa kama vile kufariki dunia.”

Amesema kwa sasa zoezi hilo tayari limekamilika katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Simiyu, Mara na Mwanza (isipokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba). Zoezi hilo linaendelea kutekelezwa chini ya kaulimbiu isemayo Kadi Yako, Kura Yako, Nenda Kajiandikishe

No comments:

Post a Comment