Na
Omary Mngindo, Ubena.
WAKULIMA
katika Kijiji cha Visakazi, Kata ya Ubena halmashauri ya Chalinze wilaya ya
Bagamoyo mkoani Pwani, wameitaka Serikali kuwatafutia suluhu ya migogoro
inayohusiana na mifugo kijijini hapo.
Wakizungumza
na Waandishi wa habari kijijini hapo, wakazi Daud Selemani, Selemani Mtonga
wakiwemo wezee maarufu John Lumoto na Mwinjuma Malano kwa niaba ya wenzao walisema
kuwa hali kijijini hapo ni mbaya kutokana na wingi wa mifugo.
"Mimi
na familia yangu tuko katika hali ngumu ya kiuchumi kutokana na kuwepo kwa wafugaji
kwenye maeneo yetu ambayo ni kwa ajili ya kilimo, kama mnavyojionea mazao yangu
yote yameliwa, mihogo imeng'olewa pamoja na miche ya minanasi," alisema
Mtonga.
Kwa
upande wake Daud amewaonesha waandishi wa habari miche ya mikorosho na migomba
ambayo imeliwa na mifugo hali iliyomfanya mkulima huyo kuangusha kilio kutokana
na uharibifu huo.
"Serikali
inatutaka vijana tujikite kwenye kilimo, tunalima lakini mwisho wa siku mifugo
inaingizwa kwenye mashamba tunapokwenda kulalamika kwenye ofisi za serikali hakuna
hatua zinazochukuliwa, hii hali isipoangaliwa inaweza kusababisha hali
mbaya," alisema Daud.
Mkazi
Lumoto aliwataka viongozi waliochaguliwa kutimiza majukumu yao na si kila kitu
aingilie Rais John Magufuli na kuongeza kwamba hatua ya rais kuingilia migogoro
inayopaswa kutatuliwa na wateule wake ni udhaifu kwa wateule hao.
Akizungumzia
migogoro ya mifugo, Ofisa wa kitengo hicho kijijini hapo Malilo Daniel alisema
kwamba, hali ni tete kutokana na mifugo kuwa mingi aliyofikia elfu hamsini,
huku eneo la kufugia likiwa eka 499 tu, wakati eka elfu nane zikiwa kwenye
hifadhi ya Wami Mbiki.
"Wastani
ng'ombe mmoja kwa mwaka anakula eka moja, hivyo kutokana na wingi huo mifugo
kijijini hapa, kwa kipindi hiki kuna kesi za mifugo zipatazo 156, hii inadhihirisha
kwamba hali si ya kuridhisha," alisema Daniel.
No comments:
Post a Comment