Tuesday, September 17, 2019

RIDHIWANI KIKWETE AKABIDHI VITAMBULISHO VYA MATIBABU BURE KWA WAZEE.

Na Shushu Joel, Chalinze.

MBUNGE wa jimbo la Chalinze, wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete amewakabidhi wazee zaidi ya 500 vitambulisho vya matibabu bure katika jimbo lake.

Akizungumza na wazee wa kata ya Lugoba mara baada ya kuwakabidhi vitambulisho hivyo Kikwete alisema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wazee wote nchi nzima wanapatiwa vitambulisho hivyo ili kuondokana na suala la kulipia huduma za Afya.

Alisema kuwa Vitambulisho hivi vitawafanya wazee wa Chalinze kutibiwa bure na bila bugudha ya aina yeyote ile.

Aliongeza kuwa Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, imejidhatiti kuhakikisha kila jambo lililoahidiwa kwa wananchi linatekelezeka kwa wakati kwa kusudi la kuwaondolea wananchi wanyonge changamoto zao kwa vitendo.

"Naipongeza Serikali yangu kwa jinsi inavyopambana na maendeleo pia utoaji wa huduma kwa wananchi wake kwani wazee wetu ni haki zao kupata Vitambulisho na wamevipata ili kupata huduma hiyo bure" Alisema Ridhiwani Kikwete.


Aidha aliongeza kuwa Wazee kupatiwa vitambulisho ni haki yao kutokana na kuwa Wazee hao walijitoa kwa hali na Mali enzi za ujana wao katika kulipambania taifa hili hivyo Serikali kuwapatia vitambulisho kwa ajili ya matibabu bure ni haki yao.

Kikwete aliwataka Wazee hao kuhakikisha wanavitunza vitambulisho hivyo ili visichakae wala wasivipoteze kwani itakuwa ni changamoto kupatikana kwa wakati.

Aidha Mbunge huyo ametoa wito kwa wauguzi wote wa halmashauri ya Chalinze kuhakikisha wanawapa kipaumbele kwa kuwapatia matibabu ya haraka ili waondoke mapema  wapate muda wa kupumzika.

Kata ambazo wazee wamepatiwa vitambulisho ni Lugoba, Msoga, Pera, Talawanda, Ubena, Miono, Vigwaza na Msata.

Kwa upande wake Muhammed Mzimba amempongeza mbunge wa jimbo hilo Ridhiwani Kikwete Kwa kuwapa kipaumbele wazee wa jimbo zima ili kuhakikisha wanapata huduma za matibabu bure katika vituo vya afya na sehemu zote zinazotoa huduma za kiafya Kwa wazee.

Aliongeza kuwa Kwa sasa wazee hao watatembea kifua mbele kutokana na jinsi serikali ya awamu ya Tano inavyowajali wazee Kwa kupatiwa huduma za afya bure.

Aidha Mzee huyo alisema kuwa mara baada ya kupokea vitambulisho hivyo vitawasaidia sana na kuhakikisha watavilinda na watavitunza ili viendelee kutumika kwenye upande huo wa Afya.

Naye Bi Fatma Musa mkazi wa Msata (62) amewaomba wauguzi kutoa matibabu bila ubaguzi ili nao wajisikie kama wanavyopatiwa huduma watu wengine wenye umri wa chini yao.

Aidha amempongeza Mbunge Ridhiwani Kikwete kwa juhudi zake za kuwapambania wazee wa jimbo lake katika kuhakikisha wanapatiwa huduma ya matibabu bure.

No comments:

Post a Comment