Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, akikata
utepe kuashiria uwashaji rasmi wa umeme katika Shule ya Msingi ya Kabeho,
iliyopo wilayani Chato, Septemba 16, 2019.
................................
Na Veronica Simba - Geita
Serikali imewaagiza watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kuwaunganishia umeme wananchi wa
vijiji vyote 11 vya Kata ya Nyankumbu iliyopo Geita mjini, kwa gharama ya
shilingi 27,000 tu kuanzia sasa.
Agizo hilo lilitolewa jana, Septemba 16 mwaka huu na Waziri
wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, wakati akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Uwanja,
Kata ya Nyankumbu, akiwa katika ziara ya kazi.
Waziri alisema, awali, Kata hiyo haikuwa katika mpango wa
umeme vijijini, ambao wanufaika wake ndiyo huunganishiwa umeme kwa gharama hiyo
lakini baada ya serikali kujiridhisha kuwa eneo hilo halina tofauti na maeneo
mengi ya vijijini, imeamua nao wapatiwe huduma hiyo kwa gharama inayotozwa
vijijini.
Aidha, Waziri aliwaagiza viongozi wa taasisi husika kwa
kushirikiana na mkandarasi anayetekeleza mradi wa umeme vijijini, awamu ya
tatu, wilayani humo, kuweka magenge 10 katika Kata hiyo na waanze kuunganishia
wananchi umeme mara moja.
Hata hivyo, Waziri Kalemani alibainisha kuwa,
watakaounganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 katika eneo hilo, ni
wale tu wateja wapya na kwamba wale ambao walikwishaunganishiwa awali kwa
gharama tofauti, hawatahusika na hawatarejeshewa fedha.
Katika hatua nyingine, Waziri aliendelea kusisitiza agizo
lililotolewa na serikali kuwa wananchi vijijini hawapaswi kulipia nguzo wala
kifaa kingine chochote isipokuwa gharama za kutandaza mfumo wa nyaya kwenye
majengo yao (wiring), ambazo ni makubaliano yao binafsi na wakandarasi
watakaowafanyia kazi hiyo.
Alitoa onyo kali kwa yeyote atakayebainika kumwambia
mwananchi kulipia nguzo au kumtoza gharama nyingine yoyote zaidi ya shilingi
27,000 tu ambayo ndiyo bei halali iliyotangazwa na serikali kwa ajili ya
kuunganishia umeme wananchi wa vijijini.
Katika ziara hiyo, Waziri pia alitembelea kijiji cha Kabeho
kilichopo wilayani Chato mkoani humo, ambapo aliwasha rasmi umeme katika Shule
ya Msingi ya kijiji hicho.
Aliwataka wanafunzi kuutumia umeme huo kwa ajili ya kuongeza
kiwango cha ufaulu shuleni hapo.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kulia),
akimkabidhi kifaa cha Umeme Tayari (UMETA), mmoja wa wanakijiji wa Kabeho
wilayani Chato, wakati wa hafla ya uwashaji rasmi umeme katika kijiji hicho,
Septemba 16, 2019.
No comments:
Post a Comment