Thursday, September 26, 2019

RC NDIKILO AWAONYA WATEKAJI WATOTO PWANI.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo akimkabidhi cheti mmoja wa wanafunzi waliohitimu darasa la saba katika  mahafali ya 14 ya shule ya Kibaha  Indepent Lisa Vicent  kushoto kwake ni  Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa shule hiyo Alhaji Yusuph Mfinanga akifuatiwa na Mkuu wa shule hiyo Charles Majani.(PICHA NA VICTOR MASANGU)

..................................
VICTOR  MASANGU, PWANI.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo amechukizwa na  vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na baadhi ya makundi ya watu wahalifu ambao wanawateka watoto wa shule.


Ametoa onyo kwa watekaji na kusema kuwa, Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoani humo ipo macho na itamshughulikia kila anaehusika na vitendo hivyo.


Aidha, amewataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama ili kuwabaini wale wote wanaofanya vitendo vya kihalifu.


Ndikilo  ametoa kauli hiyo wakati wa sherehe ya  mahafali ya 14 ya darasa la saba  katika shule ya msingi Kibaha Independent  ambapo pia amewaasa wanafunzi wote waliohitimu kutojiingiza  kabisa katika makundi ya uvutaji wa madawa ya kulevya, mahusino ya kimapenzi, uhalifu wa aina zote na badala yake wahakikishe wanakuwa wazalendo na nchi yao na kuzingatia elimu waliyopata kwa lengo la kutimiza malengo waliyojiwekea.


“Kwa kweli ndugu wazazi na walezi kwa sasa kumeanza kuingia kwa baadhi ya watu kuwateka watoto wetu wa shule na hivi karibuni kumetokea mwanafunzi mmoja wa shule ya sekondari Tumbi kutekwa na watu wasijulikana katika mazingira ya kutatanisha na kumpakia kwenye gari ndogo kisha kwenda kumtelekeza maeneo ya ubungo jijini Dar es Salaam, kwa hiyo  kwa sasa bado tunaendelea na msako kwa ajili ya kuwatafuta wahusika,”alisema Ndikilo.


Wakati huohuo, Ndikilo aliupongeza uongozi wa shule ya Kibaha Independent kwa juhudi wanazozifanya katika uboreshaji wa elimu kwa wanafunzi wao ambao wamekuwa wakifanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya darasa la saba katika ngazi ya taifa na kuwataka walimu waendelee na bidii zaidi ili waweze kushika nafasi ya kwanza katika mitihani yao waliyoimaliza hivi karibuni.


“Walimu wa Kibaha Independent kwa  kushirikiana na bodi yote ya wakurugenzi kwa kweli mnafanya kazi nzuri na serikali ya awamu ya tano itaendelea kushirikiana bega kwa began na shule binafsi lengo ikiwa ni kuhakikisha watoto wetu wote wanapata elimu ambayo itawasaidia katika siku za baadae ,”alisema Ndikilo.


Kwa upande wake Mkuu wa shule ya Kibaha Independent  Charles Majani amempongeza Rais wa awamu ya tano Dk. John Pombe Magufuli kwa kuboresh sekta ya elimu na kuiomba serikali kuwasaidia upatikanaji wa vibali kwa wakati  kwa ajili ya kuanzisha shule mpya nyingine ambayo itaweza kutoa fursa zaidi ya kutoa taaluma kwa wanafunzi bila ya kuwa na vikwazo vyovyote.

 
Naye Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa shule hiyo Alhaji Yusuph Mfinanga amewataka wazazi  na walezi kuwalinda  kikamilifu watoto wao na kuepukana na matapeli katika suala zima la ulipaji ada.
Aliwataka wazazi na walezi pia, watumie mfumo ambao umewekwa wa kufanya malipo kwa kutumia njia ya taasisi za kibenki ili kuondokana na usumbufu ambao umekuwa ukijitokeza.


Hama mmoja wa wanafunzi akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake alisema kuwa  elimu waliyoipata imewatoa ujinga na kwamba lengo lao kubwa ni kufika mbali zaidi hadi ngazi ya vyuo vikuu na kuwashukuru walimu wao ambao wameweza kushirikiana nao bega kwa bega katika kipindi chote cha miaka saba kwa kuwapatia elimu na mahalifa katika maisha yao.


Hivi karibuni  Wilayani Kibaha mkoani Pwani kulitokea tukio la kutekwa kwa mwanafunzi mmoja wa kidato cha pili katika  shule ya sekondari tumbi na watu wasiojulikana na kumtelekeza katika maeneo ya Ubungo  Jijijni Dar es Salaam.

Wanafunzi waliomaliza darasa la saba katika shule ya msingi Kibaha  Kibaha Independent wakicheza kwa furaha katika sherehe ya mahafali yao ya 14 ambayo ilihudhuliwa na viongozi mbali mabli wa serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo.

No comments:

Post a Comment