Saturday, September 28, 2019

Madini ya Bati mbioni kuanza kuuzwa nje



Tanzania iko mbioni kuandika historia ya kuuza madini ya bati nje ya nchi, ikiwa ni kwa mara ya kwanza kwa nchi kufanya hivyo.

Habari hizo njema zimetangazwa mjini Geita na Waziri wa Nishati, Dotto Biteko wakati wa maonesho ya pili ya teknolojia na uwekezaji katika sekta ya madini yanayoendelea mjini hapa.

Biteko alisema baada ya juhudi kubwa zinazofanywa na serikali katika kuhakikisha nchi inanufaika na utajiri wa madini mbalimbali nchini yakiwemo dhahabu, tanzanite, almasi, shaba, rubi, graphite na mengine, madini ya bati nayo yako mbioni kuingia katika soko la kimataifa.

Alisema katika kuchochea uchumi wa viwanda, Wizara kupitia Tume ya Madini imekwishatoa leseni mbili za usafishaji madini, moja mkoani Dodoma na nyingine Geita, huku leseni nne zikiwa kwa ajili ya uyeyushaji wa madini ya shaba na bati.

Aidha, alisema changamoto kubwa ya usafirishaji wa madini ya bati nje ya nchi inaelekea kupatiwa ufumbuzi kwani Wizara kwa kushirikiana na Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) zipo katika hatua za mwisho kuwezesha upatikanaji wa hati ya kusafirisha madini ya bati.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera aliyehudhuria maonesho ya madini mkoani Geita akiambatana na wachimbaji wadogo kutoka mkoani mwake, Michael Gaguti alisema amekuja kujifunza juu ya mafanikio ya Geita katika soko la dhahabu na pia kujifunza juu ya teknolojia za kisasa, huku akisema anaamini Kagera pia itanufaika kupitia maonesho hayo.

No comments:

Post a Comment