Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu akizungumza na wahitimu
wa vyuo vikuu wanaoishi karibu na Hifadhi ambao wametoka familia duni
waliosomeshwa na Asasi isiyo ya Kiserikali ya Africa Foundation, And Beyond
katika hafla iliyofanyika jijini Arusha ya kuwapongeza baada ya kuhitimu elimu
yao.
.......................................
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mhe.Constantine Kanyasu amewataka wahitimu waliomaliza Vyuo vikuu waliosomeshwa
kupitia mradi wa kuzisaidia familia duni katika vijiji vinavyopakana na maeneo
ya Hifadhi wakumbuke kurudi katika vijiji vyao ili wakawahudumie wananchi wa
maeneo hayo.
Pia, Amewataka wahitimu hao wakawe mabalozi wazuri
wa kutoa elimu kwa jamii zao juu ya umuhimu wa kulinda Hifadhi kwa vile wao
miongoni mwa wanufaika wa shughuli za Uhifadhi nchini.
Akizungumza kwenye hafla ya kuwapongeza wahitimu 50
katika ngazi ya Astashahada na Shadada katika kozi tofauti iliyofanyika Jana
usiku mkoani Arusha, Mhe.Kanyasu ameitaja Asasi isiyo ya Kiserikali ya Africa
Foundation kupitia kuwa ni moja ya wadau muhimu wa Uhifadhi ambao ni mfano wa
kuigwa katika kuzisaidia familia masikini.
Africa Foundationi ni Asasi inayotekeleza mradi
wake kwa kusaidia kulipa ada kwa wanafunzi kutoka familia duni zinazoishi
karibu na Hifadhi kujiunga na vyuo vikuu nchini kama inavyofanya Bodi ya Mikopo
ya Vyuo Vikuu ( HESLB).
Asasi hiyo inayoendesha baadhi ya Hoteli za kitalii
ndani ya Hifadhi za Taifa nchini na imekuwa ikisaidia familia duni kwa
kuwalipia ada wanafunzi hao ikiwa kurudisha kwa jamii kile walichopata kupitia
Hoteli hizo.
Mkopo huo ni tofauti na ule wa HESLB ambapo mara
baada ya kusomeshwa na Africa Foundation wanafunzi hao hulipa mkopo huo kwa
kuihudumia jamii alikotoka kulingana na kozi aliyoisomea badala ya kurudisha
pesa.
Naye, Waziri wa Habari, Utalii na Mambokale,
Mhe.Mahamoud amewataka wahitimu hao wakaitumie elimu hiyo kwa kuwasaidia vijana
wengine waweze kutambua thamani ya elimu katika maisha yao
” Nendeni huko mkaibadilishe jamii yenu ianze
kutambua umuhimu wa kutunza maliasili tulizonazo, alisisitiza Mhe, Waziri
Kombo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa mkoa Arusha, Jerry
Muro amewataka wanafunzi hao wakaitumie vizuri elimu yao kwa kuanza kuzibadili kifikra
familia zao pamoja na jamii kuhusu umuhimu wa kutunza Hifadhi na kuachana na
vitendo vya ujangili ili watalii waendelee kuja nchini
” Elimu yenu ikawe silaha kwa wale wote
wanajihusisha na vitendo vya ujangili” alisisitiza Mhe.Muro.
Naye Mkurugenzi wa Africa Foundation kwa nchi za
Africa Mashariki, Dkt. Mkomeni Mgonho amesema lengo la kutoa msaada huo ni
kuzifanya familia hizo kuthamini na kuona thamani ya shughuli za Uhifadhi.
Aidha, Amesema kuwa pia ni mchango wao
wanaourudisha katika jamii kwa kile wanachopata kupitia Hoteli za kitalii.
Mbarouk Salum ambaye ni mhitimu wa fani ya Udaktari
katika Chuo Kikuu kishiriki cha Muhimbili amesema kitendo cha Asasi hiyo
kuwasaidia kwa kuwalipia ada ni moja ya alama kubwa za matumaini kwa familia
hizo ambapo zitaweza kubadili maisha kwa kuandaa kizazi bora kitakachopenda na
kuthamini shughuli za Uhifadhi.
Africa Foundation imesaidia kuwalipia ada wanafunzi
45 wa Kitanzania pamoja wanafunzi wa 5 wa kutoka nchini Kenya wote wakiwa
wanaishi kwenye vijiji vinavyopakana na Hifadhi.
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu (wa pili kulia) akiwa na
Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya kale wa Zanzibar, Mhe. Mahamoud Kombo
wakiwa kwenye picha ya pamoja na mhitimu wa Chuo Kikuu mara baada ya kukabidhiwa
cheti chake.
Baadhi ya
wahitimu wa vyuo vikuu wanaoishi karibu na Hifadhi ambao wametoka katika
familia duni waliosomeshwa na Asasi isiyo ya Kiserikali ya Africa Foundation,
And Beyond wakiwa wamesimama wakati Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mhe.Constantine Kanyasu akiwa anawasili ukumbini katika hafla iliyofanyika
jijini Arusha ya kuwapongeza baada ya kuhitimu elimu yao.
No comments:
Post a Comment