Monday, September 30, 2019

AHUKUMIWA JELA MAISHA, KWA KULAWITI, KUBAKA MTOTO WA MIAKA 10.

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

MAHAKAMA ya Wilaya ya Lindi, Mkoani hapa, imemuhukumu kifungo cha maisha Gerezani, Emmanuel Thomasi Msemakweli (29), mkazi wa Mtaa wa Kariakoo, Kata ya Rasbura, Manispaa ya Lindi, baada ya kukutwa na hatia ya makosa mawili.

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 27 Septemba 2019 na Hakimu mkazi wa Mahakama hiyo, Franco Kiswaga, baada ya mshtakiwa kukutwa na makosa mawili likiwemo kubaka na kulawiti Mtoto wa kike na mwanafunzi mwenye umri wa miaka 10, (jina limehifadhiwa).

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Hakimu Kiswaga alimuuliza mshtakiwa kwa nini Mahakama isimpe adhabu kali kutokana na makosa aliyoyafanya dhidi ya mlalamikaji, ambapo aliomba imuonee huruma kwa madai ni mkosaji wa mara ya kwanza na alifanya kosa hilo baada ya kupitiwa na Ibirisi.

Baada ya utetezi huo, Mwanasheria wa Serikali Yahaya Gumbo akisaidiana na Godfrey Mramba waliiomba Mahakama kumpa mshitakiwa adhabu kali ili iwe fundisho kwake na wengine walio na tabia ya aina hiyo.

Hakimu Kiswaga baada ya kusikiliza maombi ya pande zote mbili, alisema anakubaliana na maombi yao, lakini kutokana na Sheria kumfunga mikono, huku akitumia vifungu 130 (1), (2) (a) na 131 (1) kanuni ya adhabu sura ya 16/2002 kutoa adhabu, alimuhukumu kutumikia kifungo cha miaka (30) kwa kosa la kubaka.

Pia, Hakimu Kiswaga akitumia kifungu namba 154 (1) (a) kanuni hiyo ya adhabu sura ya 16/2002 katika kesi hiyo namba 37/2019, alimuhukumu kifungo cha Maisha, na kwa kuwa adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, Emmanuel Thomas Msemakweli atalazimika kuishi Gerezani maisha yake yote hapa duniani.

Awali ilidaiwa Mahakamani hapo na wanasheria wa Serikali, Yahaya Gumbo na Godfrey Mramba, kuwa mshitakiwa kwa muda, siku na nyakati tofauti, huku akifahamu anacho kifanya ni kosa, alimbaka Mtoto wa kike na mwanafunzi mwenye umri wa miaka kumi (majina likiwemo la Shule anayosoma yamehifadhiwa).

Wanasheria hao waliiambia Mahakama kuwa hali hiyo ilifahamika baada ya walimu wake na mama yake kuona mabadiliko, yakiwemo utembeaji wake na kushuka kwa maendeleo yake Shuleni.

Aidha, walieleza kwamba kufuatia hali hiyo, walimu na mzazi wake, walimuhoji na kuelezea kile kinachomsibu, kisha kuchukuwa hatua ya kumpeleka Hospitali kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu na kubainika kuingiliwa sanjari na kinyume na maumbile.

Wanasheria hao walieleza kuwa baada ya kubaini hilo, walimu wakishirikiana na mama wa mwanafunzi huyo walitoa taaifa kwa vyombo husika vya Serikali, ndipo mshitakiwa alipokamatwa.

No comments:

Post a Comment