NAIBU Waziri wa Kilimo Omari
Mgumba akizungumza na watumishi wa Halamashauri ya wilaya ya Pangani wakati wa
ziara yake kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) Jumaa Aweso ambaye pia
ni Naibu Waziri wa Maji na Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Pangani, Zainabu Abdallah
.....................................
NAIBU Waziri wa Kilimo Omari Mgumba amewataka walimu
wa shule za Msingi na Sekondari waache kutumia kilimo kama adhabu ya kuwapa
wanafunzi wakati wanapokosea kwani inawajengea tafsiri mbaya kwa jamii na
baadae wanapokuwa, wanachukia kilimo.
Mgumba alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa ziara yake
wilayani Pangani ambapo alisema kwamba kuna tabia ambayo imejengeka kwa walimu
hao kwamba mtoto anapokosea anaambiwa leo utakwenda kulima siku nzima,
utakwenda kumwagilia hali ambayo inapelekea baadae wakikua wanakuwa hawahitaji
kilimo kwa sababu awali waliona kama adhabu.
Alisema hapana, suala hilo sio jema na ndio maana wao
wanasema kilimo ni uti wa mgongo lakini watafungamanisha kilimo na elimu ili
watoto tokea anakuwa ajue kwamba nchi hii uchumi wake unategemea kilimo.
“Hivyo ninapoambiwa niwe na tuta la mchicha sio adhabu
bali ni sehemu ya kuniandaa kielimu nije kujitegemea au nije kuajiri wengine
kwenye mashamba yao kwani bila kufanya hivyo tutakuwa tunaimba kitu kingine
wakati uchumi wetu unategemea kilimo”Alisema Naibu Waziri huyo.
Naibu Waziri huyo alisema kwamba mkakati wa serikali ni
kuimarisha kilimo hivyo wataendelea kufungamanisha elimu na kilimo chao.
Akizungumzia Kilimo cha Minazi wilayani humo Naibu Waziri
huyo alisema kwamba kilimo cha minazi ni kweli hawajapata ufumbuzi wa magonjwa
yake kwa miaka zaidi ya 30 sasa, ambayo yanasababsihwa na mabadiliko ya tabia
ya nchi.
Alisema pia hilo linatokana na kukubali kuletewe mbegu ya
kisasa ambayo haiendani na mazingira ya nchi hivyo kama Taifa wameendelea
kuimarisha vituo vyao vya utafiti hasa cha utafiti wa minazi mikocheni lengo ni
kuanza kurudi kwenye kuzalisha miche kutumia minazi ya asili inayokabiliana na
hali ya hewa na ikolojia ya ya nchi yetu .
“Na sasa tumeanza kuzalisha kitalu cha miche asili
Bagamoyo na itasambazwa nchi nzima kwa lengo la kupanda na hatimaye kuweza
kurejesha minazi hiyo ”Alisema.
Akizungumzia udogo wa bei ya nazi nchini Naibu Waziri huyo
alisema kwamba nazi zinauzwa bei ndogo na imeendelea kuwa ndogo ni kutokana na
ushindani uliopo kwenye soko la ndani, kanda na kimataifa kwa sababu ya bidhaa
mbadala.
“Hivyo kila nazi ikipanda bei, watu wanakwenda kutumia
mafuta lakini kila tunapoacha kutumia nazi na kutumia mafuta na kwenda kwenye
chukuchuku wanapunguza mahitaji ya nazi ”Alisema.
Hata hivyo alisema kwamba wanakuja na mkakati wa kuanzisha
viwanda ambavyo vitaongeza thamani bidhaa hiyo ili kupanua soko la nazi hapa
nchini na mbegu za nazi ambazo zinaweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya
nchi huku akieleza kwamba wakienda kuongeza thamai tatizo hilo litakwisha.
Katika hatua nyengine Naibu Waziri huyo aliwataka
watanzania kuendelea kutumia nazi kwani wanapoendelea kuitumia zaidi wanaongeza
mahitaji na soko la nazi litakuwa kubwa huku akisistiza kwamba watakaendelea
kutumia mafuta bei ya nazi itashuka.
Awali akizungumza wakati wa ziara hiyo Mbunge wa Jimbo la
Pangani (CCM) Jumaa Aweso alisema kwamba zao la nazi limeathiriwa na maradhi kwa
muda mrefu na bado tiba yake haijapatikana miaka 30 sasa.
Alimwambia Naibu Waziri Mgumba kwamba ugonjwa huo umekuwa
haupati ufumbuzi kama lilivyokuwa gonjwa la ukimwi hivyo walimuomba watafiti na
watalamu wafanye utafiti ambao utafika mwisho na wenye manufaa na kuweza
kurudisha uchumi wake.
Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM)
Jumaa Aweso ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji kulia akimueleza jambo Naibu
Waziri wa Kilimo Omari Mgumba wakati wa ziara yake wialayani humo.
MKUU wa wilaya ya Pangani Zainabu Abdallah
akizungumza wakati wa ziara hiyo kushoto ni Katibu Tawala wa wilaya ya Pangani,
Mwalimu Hassani Nyange.
No comments:
Post a Comment