WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezielekeza mamlaka
husika ziwachukulie hatua za kinidhamu watu wote ambao hawakutekeleza majukumu
yao ipasavyo kufuatia tukio la ajali ya moto iliyotokea Agosti 11, 2019 mkoani
Morogoro na kusababisha vifo vya watu 104, majeruhi pamoja na uharibifu wa
mali.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Septemba
13, 2019) , wakati akiahirisha mkutano wa 16 wa Bunge la 11, Bungeni jijini
Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi tarehe 3, Novemba mwaka huu.
“Baada ya tukio hilo la kusikitisha tarehe 12
Agosti 2019niliunda Kamati Maalumu kwa lengo la kufanya uchunguzi wa kina
kuhusu ajali hiyo iliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.”
“Lengo lilikuwa kufahamu chanzo cha ajali,
mazingira baada ya ajali na hatua gani zichukuliwe kuzuia matukio kama haya
sambamba na kuwawajibisha wale wote ambao hawakutekeleza wajibu wao ipasavyo
kabla na baada ya ajali kutokea.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo
kuwashukuru madaktari na wahudumu wa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro na Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili nawadau wote ambao walishiriki kuokoa maisha ya
waathirika wa ajali hiyo tangu ilipotokea.
“Nawasihi Watanzania wenzangu tujifunze kutokana na
ajali hiyo iliyotokea Morogoro na hivyo kuepuka mikusanyiko ya aina hiyo katika
maeneo ya ajali. Aidha, tujenge nyoyo za huruma na kuwa wepesi wa kutoa msaada
kwa waathirika wa ajali badala ya kutumia kama fursa za kujinufaisha isivyo
halali.”
No comments:
Post a Comment