NA
MWAMVUA MWINYI, KIBAHA.
MKUU
wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amemuagiza Mganga Mkuu wa mkoa (RMO)
kuandika barua kuomba kibali Wizara ya afya ili kutuma tume kuchunguza mtoto
aliyechomwa sindano na kupooza mguu.
Ndikilo
aliyasema hayo mjini Kibaha wakati alipofanya mkutano wa wazi wa kusikiliza
matatizo na kero mbalimbali za wananchi ambapo mama wa mtoto huyo Asha Juma
alitoa kilio cha mwanae mbele ya mkuu huyo wa mkoa.
Akielezea
juu ya tukio la mwanae aitwaye Abbas Msosa (14) ambaye anasoma kidato cha
kwanza shule ya sekondari Bundikani Wilayani Kibaha, Asha Juma, alisema kuwa
mwanaye alikuwa akiumwa na alimpeleka kituo cha afya mkoani kwa ajili ya
matibabu.
Asha
alisema kuwa alipokuwa anapatiwa matibabu alichomwa sindano ambayo ilimsababishia
maumivu na kusababisha mguu wake kupooza kutokana na kuchomwa sindano ya
Quinine alipokuwa akiumwa Malaria miaka tisa iliyopita.
“Naomba
suala langu lishughulikiwe kwani hata majibu ninayopewa na waliohusika na suala
la mtoto wangu wananipa majibu ambayo hayaridhishi ninachokitaka ni kupata haki
ya mtoto wangu ambaye amepata matatizo kutokana na matibabu aliyopewa,” alisema
Asha Juma.
“Nimezunguka
sana kwenda kwenye kituo hicho cha afya cha Mkoani lakini sipati majibu
yanayoeleweka nakuomba unisaidie nateseka sana kwani nahangaika na mwanangu na
sina msaada wowote nakuomba unisaidie nipate haki ya mwanangu,” alisisitiza kwa
masikitiko Bi Asha Juma.
Kwa
upande wake mkuu wa mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo alisema kuwa suala
hilo analifahamu kuwa mtoto wake alipatiwa matibabu kwenye kituo hicho cha afya
na baada ya mwanae kuchomwa sindano alipatwa na tatizo hilo.
“Lifanyiwe
kazi na kama kuna mtu ambaye alizembea na kusababisha tatizo hili ili hatua za
kinidhamu zichukuliwe kwani kwa sasa hatuwezi kutoa majibu kujua kama ni uzembe
au la hili likitolewa ufafanuzi na wataalamu itakuwa ni vizuri ili liweze
kwisha kwani lazima kuwe na majibu ambayo yatakuwa ni ya kitaalamu,”alisema
Ndikilo.
Alisema
kuwa suala hilo limekuwa la muda mrefu sana na mama huyo amekuwa akihangaika
sana na ameshafika ofisini kwake mara kwa mara na ameshamsaidia hivyo kuna haja
ya kuhakikisha linafikia mwisho ili naye aweze kuridhika kwani anaona kama
hajapata haki yake.
No comments:
Post a Comment