Thursday, September 19, 2019

WAZIRI MPINA ATOA MIEZI MITATU KWA FETA NA TAFIRI KUWASILISHA TAARIFA ZA WAHITIMU WA FETA.

 
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, akizungumza na wafanyakazi wa Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) alipotembelea Makao makuu ya FETA, Mbegani wilayani Bagamoyo jana Septemba 18, 2019.
..................................

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametoa miezi mitatu kwa Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) pamoja na Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) kuwasilisha ofisini kwake taarifa za wahitimu wote wa FETA ili kujua wako wapi, na wanafanya nini lengo likiwa kubaini ikiwa elimu inayotolewa na FETA inawanufasha au la.


Mpina ametoa agizo hilo jana Sepemba 18, alipotembelea Makao makuu ya Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi iliyopo Mbegani wilayani Bagamoyo, ambapo ametaka taarifa hizo za wahitimu kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.


Alisema serikali inatoa elimu kwa vijana ili waweze kunufaika na elimu hiyo na kwamba ili kujua kama wamenufaika nayo au la ufuatiliaji ufanyike sehemu walizoenda na kazi wanazofanya.


Alibainisha kuwa, vijana wengi wanapata elimu ya uvuvi na ufugaji lakini wakimaliza masomo hawaendi kufanya kazi walizosomea na badala yake wanaovua samaki na kufuga ni watu ambao hawakupata elimu hiyo.


Aliongeza kuwa, kupata taarifa zao kutaisadia Serikali kujua changamoto wanazokabiliana nazo ili kuboresha kwenye mapungufu wakati wa utoaji wa elimu na uwezeshaji kwa vijana.


Hata hivyo alitoa wito kwa vijana wanaoendelea na masomo kutumia taaluma wanazopata katika vyuo vilivyo chini ya FETA ili kujiongezea kipato hali itakayosaidia kupunguza makali ya ada.


Alisema vijana wanapswa kuwa wabunifu ndani ya fani yao ambapo wanaweza kutumia muda wa likizo kufundisha watu wengine maswala ufugaji samaki na kuhudumu kwenye taasisi zinazoshughulika na uvuvi na ufugaji wa samaki kwa gharama nafuu na kwamba kufanya hivyo kutawasaidia kupata fedha za ada ili waendelee na masomo.


Awali Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi, (FETA) Yahaya Mgawe, alisesema wahitimu wao wameweza kutawanyika sehemu mbalimbli na kufanya kazi za aina tofauti.


Aidha, aliongeza kwa kusema kuwa, Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi, wanao wakafunzi wenye taaluma za juu kuweza kuwafundisha vijana lakini bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa cheti cha uthibitisho wa viwango vya mafunzo (STCW)


Alisema shughuli za uvuvi wanazofanya zinahusisha bahari kuu na hivyo cheti cha uthibitisho (STCW) kitawasaidia kufanya shughuli zao kimataifa kwenye bahari kuu.


Nae Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Bi Zainabu Kawawa, wakati akimkaribisha Waziri kuzungumza, alisema wilaya ya Bagamoyo sehemu kubwa eneo lake imezunguukwa na maji ikiwemo mito, na bahari na kufanya shughuli kubwa ya wakazi wa wilaya hiyo kuwa ni uvuvi.


Kutokana na hali hiyo, Mkuu huyo wa wilaya alimuomba Waziri wa Mifugo na Uvuvi, kutafuta wadau watakaoweza kujenga kiwanda cha Samaki wilayani humo ili samaki wanaovuliwa na wakazi wa Bagamoyo na wale wanaovuliwa na Chuo cha Uvuvi Mbegani wapate sehemu ya kusindikwa kuongeza thamani ya zao la samaki wilayani humo.


Aliongeza kwa kusema kuwa, wilaya ya Bagamoyo ni wilaya yenye viwanda vingi lakini hakuna kiwanda cha samaki hali ya kuwa eneo lake kubwa limezunguukwa ya maji mito na Baharai.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi alikuwa katika ziara ya siku moja wilayani Bagamoyo ili kukutana na Wakala wa Elimu na Uvuvi (FETA) na taasisi nyingine zinazohusiana na uvuvi ili kuangalia changamoto zinazoikabili sekta ya uvuvi na kuzishughulikia.
 
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Bi Zainabu Kawawa, akizungumza wakati wa kumkaribisha Waziri wa Mifugo na Uvuvi (wa pili kushoto). Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Yahaya Mgawe, akizungumza mbele ya
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina
 
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, (kushoto) akipokelewa na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Zainabu Kawawa, mara tau alipowasili Makao Makuu ya Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Mbegani.
 
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, (kushoto) akisani kitabu cha wageni alipoingia ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Mbegani wilayani Bagamoyo.
 
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, (katikati) akitembezwa katika eneo la Chuo cha Uvuvi mbegani, kulia ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Yahaya Mgawe, na kushoto ni Katibu Tawala wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni.
 
 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Yahaya Mgawe, (kushoto) akimuonyesha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina baadhi ya Meli za uvuvi zilizopo Chuo cha Uvuvi Mbegani, kulia ni Katibu Tawala wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni.
 
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Yahaya Mgawe, katika eneo la Chuo cha Uvuvi Mbegani Bagamoyo, ambapo ndio Makao Makuu ya FETA, wa pili kushoto ni Katibu Tawala wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni.
 
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, akisikiliza maelezo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Yahaya Mgawe, Kwenye karakana ya kutengeneza Boti, katika eneo la Chuo cha Uvuvi Mbegani Bagamoyo.
 
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, akiwapa chakula Samaki wanaofugwa katika Chuo cha Uvuvi Mbegani, katikati ni Katibu Tawala wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni.         

No comments:

Post a Comment