Sunday, September 1, 2019

Programu Ya Kitalu Nyumba Yawapa Hamasa Vijana Kushiriki Kwenye Sekta Ya Kilimo


Na; Mwandishi Wetu
Programu ya ukuzaji ujuzi kwa vijana kupitia teknolojia ya Kitalu nyumba (Green house) inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imewapa hamasa vijana kushiriki kwa wingi kwenye sekta ya kilimo ikiwa ni chanzo cha kimoja wapo cha ajira nchini.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama wakati wa Ziara yake ya kukagua maendeleo ya mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vijana kupitia teknolojia ya Kitalu Nyumba, Mkoani Iringa.

Waziri Mhagama alieleza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu iliamua kuanzisha programu hiyo kwa lengo la kuwawezesha vijana kushiriki kwa wingi kwenye masuala ya kilimo ili waweze kujiajiri wao wenyewe na kuajiri vijana wenzao kupitia teknolojia hiyo.

“Mradi huu unatekelezwa kwenye Halmashauri 185 nchini katika awamu hii ya kwanza ikiwa na lengo la kuwawezesha vijana kuwa na ujuzi pamoja na stadi za kilimo cha kisasa kupitia kitalu nyumba ambacho kina tija katika kuwapatia mazao bora na mengi yatokanayo kwenye eneo dogo,” alieleza Mhagama

Alieleza kuwa Serikali imeendelea kuwawezesha na kuwajengea uwezo vijana wa masuala ya ukuzaji ujuzi ili waweze kuongeza tija kwenye shughuli wanazozifanya na zitakazo wakwamua kiuchumi.

“Vijana wanaweza kupata ajira bora katika kilimo endapo watawekewa mazingira bora kama kuimarisha teknolojia na mbinu za kilimo,” alisema Mhagama.

Hata hivyo aliwasihii vijana kuhakikisha wanatunza vitalu nyumba hivyo kwa kuwa watanufaika navyo na vitawasaidia kufanilisha malengo yao sambamba na kuleta maendeleo endelevu katika sekta ya kilimo.

Aidha alitoa wito kwa wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakiksha wanawasilisha njia bora zaidi za kuwapata vijana stadi zitakazo wajengea uwezo kupata teknolojia za kisasa zitumikazo katika kilimo pamoja na kuwapatia mitaji ambayo itawawezesha kujenga vitalu nyumba vyao binafsi.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Venerose Mtenga alisema kuwa Ofisi hiyo inatekeleza programu mbalimbali zitakazo wawezesha vijana kupata ujuzi na stadi stahiki zitakazo wasaidia kuondokana na changamoto ya ajira.

Naye Mratibu wa Mradi huo katika Halmashauri ya Iringa Vijijini Bw. Daniel Mlay alisema kuwa jumla ya vitalu nyumba vinne vimejengwa na vijana 431 wameweza kunufaika na mafunzo hayo.

“Tutaendelea kuwahamasisha vijana washiriki kwa kikamilifu katika mradi huu kwa kuwa una manufaa mazuri kwao,” alisema Mlay  

Pia mmoja wa vijana walionufaika kupitia Mradi huo Bw. Ramadhani Haule alieleza kuwa mradi huo wa Kitalu Nyumba umewasaidia kupata elimu bora ya kilimo na umesaidia vijana kuondoka kwenye makundi ya wasiokua na ajira.

“Tunaishukuru Serikali kwa kutuamini na kutupatia ujuzi huu, tunaahidi tutaendelea kushirikiana vijana wengi ili kujikwamua kiuchumi,” alisema

Katika ziara hiyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama alitembelea Vitalu Nyumba vilivyopo katika eneo la Ihemi na Halmashauri ya Mafinga.

No comments:

Post a Comment