Baraza la madiwani wanaounda
Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa pwani, wamefanya maamuzi magumu
likiwemo kufuatilia kwa karibu mifugo ya Ng’ombe iliyovamia mashamba na
kuharibu mazao ya wakulima.
Akijibu maswali ya papo kwa papo
katika kikao cha robo ya nne ya mwaka kilichofanyika katika ukumbi wa flex
Garden Kiguza Mkuranga, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Juma Abeid alisema
wametenga shilingi milioni 17 ili kuendesha operesheni endelevu kubaini Ng’ombe
walioingia kinyemela ndani ya Wilaya ya Mkuranga.
Akiendelea kufafanua malengo ya
opereshi hiyo amesema lengo kuu la kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa Wilaya ya
Mkuranga inakuwa salama kwa kuwaondoa Ng’ombe wote na kuwarejesha walikotoka
ili kuepusha mapigano kati ya wakulima na wafugaji.
Juma ambaye pia ni Diwani wa kata ya
Magawa alifika mbali zaidi kwa kuweka bayana changamoto sugu ya kuvamiwa maeneo
ya ardhi na Wilaya jirani za Kisarawe, Temeke, Kibiti, Ilala na Kigamboni huku
wakimuomba Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi William Lukuvi kufika na wataalam
wake ili kutatua migogoro hiyo.
Aidha ameiomba Timu ya uhakiki
wakulima wa Korosho Wilayani humo kwenda mashambani ili kujiridhisha uwepo wa
Kangomba huku akitoa mfano wapo ambao wa kilo 300 bado hawajalipwa kwa
kisingizio hicho cha kangomba.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mhandisi Mshamu Munde aliwahakikishia
Madiwani suluhisho la migogoro ya Wafugaji na Wakulima itafikia tamati karibuni
kufuatia maboresho ya sheria ndogo ya mifugo inayosubiri kupitishwa na Wizara
ambayo itatoa adhabu ya kutaifisha na kupigwa mnada mifugo inayozagaa.
Munde ambaye ni katibu wa kikao hicho
alitangaza uwepo wa kikao cha wadau wa muhogo wiki hii ambacho kitawashirikisha
wanunuzi na Mashirika mbali mbali katika sekta ya kilimo cha muhogo.
No comments:
Post a Comment