Thursday, August 3, 2023

DKT. MOLLEL ASISITIZA KUWEPO MFUMO MMOJA WA TAARIFA KATIKA SEKTA YA AFYA

Na Rayson Mwaisemba WAF- DSM


NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ametoa wito kwa Asasi ya TAHIA kutafakari juu ya kuwa na mfumo mmoja wa taarifa katika vituo vyote kuanzia ngazi ya Hospitali ya Taifa mpaka kwenye zahanati ili kusaidia kuokoa gharama za matibabu kwa mwananchi anayehitaji huduma hasa katika kipindi cha Rufaa.


Dkt. Mollel amesema hayo Jijini Dar es Salaam, katika uzinduzi wa Asasi ya Tanzania Health Information Agency (TAHIA) inayoundwa na Wataalamu wa teknolojia ya Mawasiliano yenye lengo la kuweka rasilimali watu pamoja, rasilimali fedha, teknolojia ili kwa pamoja kuondoa changamoto iliyopo ya mifumo mingi inayoshindwa kubadilishana taarifa kutoka kituo kimoja kwenda kingine.


Amesema, Mfumo huo wa taarifa za mgonjwa utaokuwa unasomana, utahusisha mpaka taarifa za fedha katika vituo, lakini pia huduma zinazotolewa kwa wagonjwa wanaotumia Bima ya afya jambo litalosaidia kuboresha huduma kwa wananchi na kupunguza upotevu wa mapato katika vituo yanayofanywa na watumishi wasio waadilifu. 


Aidha, Dkt. Mollel amesema kuwepo kwa mfumo mmoja unaosomana katika Sekta ya Afya kutasaidia kuboresha matumizi ya taarifa (data) katika ngazi ya vituo na katika ngazi ya Viongozi wa juu wa Sera ili kusaidia kufanya maamuzi sahihi ikiwemo kwenye eneo la kutenga fedha.


Sambamba na hilo, Dkt. Mollel ametoa onyo kwa Wataalamu wanaolenga kutofautisha Sekta ya Afya katika utendaji na kusisitiza kufanya kazi kwa pamoja kwa kushirikiana ili kumhudumia mwananchi aliyechini bila changamoto yoyote. 


Kwa upande mwingine, Dkt. Mollel amewataka Wadau katika Sekta ya Afya kupunguza fedha zinazotumika kwenye mafunzo, semina na warsha na kuelekeza bajeti kubwa zaidi kwenye maeneo yanayoonekana na kugusa zaidi changamoto za mwananchi wa chini mwenye uhitaji wa huduma. 


Kwa upande wake Rais wa TAHIA Bw. Sosthenes Bagumhe amemshukuru Mhe. Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel kwa ushauri alioutoa na kusisitiza tayari TAHIA imeanza kulifanyia kazi suala la kuunganisha mifumo na kuifanya iweze kubadilishana taarifa kwenye vituo kuanzia taifa mpaka zahanati ili kuondoa hadha kwa wananchi. 


Nae, Mkurugenzi wa Tehama Wizara ya Afya Bw. Ilomo Silvanus amebainisha kuwa, moja kati ya vipaumbele 14 katika Sekta ya afya vinaelekeza kuimarisha ubora wa huduma kupitia Tehama hivyo kama msimamizi wa eneo hilo atahakikisha kipaumbele hicho kinatekelezeka ipasavyo.


Bw. Eric Kitali, Mkurugenzi wa Tehama Ofisi ya Rais TAMISEMI amesema, Sekta ya afya ni moja na kuahidi kuendeleza ushirikiano na mshikamano uliopo kati ya Wizara ya Afya na OR TAMISEMI hasa katika eneo la mifumo ili iweze kuleta tija kwa wananchi wanaohitaji huduma bila kuwagharimu pasipo na sababu za msingi.





 

No comments:

Post a Comment