Thursday, August 3, 2023

TAZAMA MAMBO 6 YA TIF YANAYOISAIDIA SERIKALI.

Na Rashid Mtagaluka

TANGU serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itoe ruksa ya kuanzishwa kwa asasi mbalimbali za kiraia katika historia yake, The Islamic Foundation *(TIF)* ndiyo taasisi pekee ya Kiislamu inayojipambanua kuwa na dhamira ya dhati ya kuisaidia serikali kwa vitendo katika vita dhidi ya Ujinga, Umasikini na maradhi.

*TIF* ambayo makao makuu yake mkoani Morogoro ilianzishwa mwaka 1996 huku ikijulikana kwa jina la Morogoro Islamic Foundation ambayo pamoja na mambo mengine, ilijikita katika ujenzi wa misikiti, kulea yatima pamoja na kusaidia walemavu na watu wasiojiweza.


Uchunguzi wa kina uliofanywa na mwandishi wa makala haya umebaini kuwa, baada ya kuona mafanikio na faida kubwa wanayoipata wananchi wa mkoani Morogoro bila kujali itikadi zao za kidini na kisiasa, busara na hekima za Mwenyekiti wake Alhaj Aref Nahdi pamoja na wasaidizi wake, zikawasukuma kubadilisha jina na kuiita The Islamic Foundation, bila shaka lengo likiwa ni kuinufaisha zaidi jamii kubwa ya watanzania.

Sio lengo langu kutumia jukwaa hili kuelezea kwa kina malengo ya *TIF* hapana, bali nia yangu nikuoneshe jinsi hawa jamaa licha kwamba ni taasisi ya Kiislamu, lakini wanafanya kazi kubwa katika kuisaidia serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.


*Kwanza eneo la Habari.* Sote tunajua kwamba dunia ya leo habari imekuwa ni moja ya tasnia chache zenye nguvu kubwa na thamani nzito kiasi kwamba, nchi zilizoendelea na zisizoendelea, zimeshindwa kuidhibiti.


Kushindwa huko kunatokana na ukweli kwamba, vyanzo mbalimbali vya habari vimegeuka kuwa nyenzo muhimu katika kuongoza na kuelekeza mitazamo, fikra na mawazo ya watu kwenye masuala anuwai ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.


Vyombo vya habari vimekuwa na nguvu kubwa duniani kiasi cha kusababisha baadhi ya watu kudhani na kutamani uwe ni mhimili wa nne wa dola, mbali na Mahakama, Bunge na Serikali.


Umuhimu huu wa teknolojia ya habari na mawasiliano ndiyo ukaufanya uongozi wa *TIF* chini ya Mwenyekiti Alhaj Aref na Mkurugenzi Mtendaji wake Alhaj Sheikh Ibrahim Twaha uwekeze kwenye nyanja hiyo kwa lengo la kuisaidia jamii ya Waislamu, lakini pia kuhakikisha taarifa za uzinduzi na uendelezaji wa miradi mbalimbali ya serikali zinawafikia watanzania kwa wakati kupitia Radio Imaan, Tv Imaan pamoja na gazeti la kila wiki la Imaan.


Pamoja na kuwepo kwa baadhi ya watu kuwa na mtazamo tofauti juu ya vyombo vya habari vinavyomilikiwa na *TIF* , lakini ukweli utabaki pale pale kwamba, tangu kuanzishwe kwa Radio mwaka 2002, TV mwaka 2012 na Gazeti Imaan mwaka 2015, idadi kubwa ya watanzania wamenufaika, kwa sababu vyombo hivi vimejikita katika kutoa elimu bila mipaka.


*Amani na utulivu.* Hakuna kiongozi yeyote wa nchi duniani anayeweza kuongoza nchi yenye watu wa vurugu ambao nyoyo zao zimekosa rutuba ya mawaidha yanayowajengea hofu juu ya Mola wao Muumba.


Kwa kulijua hili, uongozi wa The Islamic Foundation umefanya kila linalowezekana kujenga nyumba za ibada (misikiti) 1612 nchi nzima pamoja na kusambaza walimu na maimamu wanaofundisha namna nzuri ya kuhamiliana na jamii hata isiyo ya Kiislamu ili kulinda umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa!


*Huduma za afya.* Nani hajui kwamba afya ndiyo mtaji pekee unaomnufaisha yeyote katika maisha ya hapa duniani? Ndiyo maana serikali ya awamu ya kwanza iliyokuwa ikiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere ilitangaza maradhi kuwa ni ADUI mmojawapo wa maendeleo yetu.


Katika kile kinachoweza kutafsirika kama uzalendo kwa nchi yao, uongozi wa TIF chini ya mwenyekiti Aref umewahi kuendesha kambi maalum za matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kugharimu kiasi cha shilingi Milioni 750 za Kitanzania.


Kwa kiongozi mwingine asiye na nia njema, pesa hizi zingemtosha kuendesha maisha yake binafsi, familia yake na viongozi wenzake wa taasisi, lakini kwa Aref Nahdi haikua hivyo!


Aidha kuna zahanati mbili kubwa mkoani Morogoro ninazozifahamu, moja iko Mikumi wilayani Kilosa na nyingine ambayo inafanyiwa ukarabati iwe kituo cha afya iko Manispaa ya Morogoro, lengo likiwa ni kuipunguzia mzigo serikali ya Rais Samia wa kuhudumia wananchi wake.


*Jambo jingine ni elimu.* Baada ya kubaini serikali inahitaji kusaidiwa katika eneo hili, *TIF* ikaona potelea mbali, ebu iisaidie serikali na nchi kwa ujumla kwa kuanzisha shule tano za msingi na shule mbili za sekondari ambazo zinapokea wanafunzi wote bila ubaguzi huku gharama yake ikimzingatia zaidi mwananchi mwenye kipato Cha chini.


Mbali na shule za awali, msingi na sekondari, *TIF* wana Maahad sita kikiwemo na Maahad Imaan cha mjini Morogoro kilichoanzishwa mwaka 2018 na uzinduzi wake rasmi umefanyika Jumapili ya Julai 30,2023, lengo ni kutoa wahitimu watakaolisaidia Taifa katika kujenga nchi yenye maadili pamoja na kuhubiri amani na utulivu wakati wa utoaji elimu ya dini.


*Huduma za kijamii na misaada ya kiutu* . Hili ni eneo jingine muhimu ambalo taasisi nyingi hulisahau. Mpaka sasa *TIF* inajivunia kuhudumia na kuwalea yatima 889 nchi nzima jambo ambalo linapaswa kuigwa na taasisi nyingine.


Mara nyingi taasisi tulizonazo badala ya kuisaidia serikali na jamii kwa ujumla, zenyewe zimejigeuza mzigo kwa kuendekeza tabia ya kuomba omba kiasi ambacho hata misaada ya wafadhili wanayoipata inashindwa kuwafikia walengwa ipasavyo.

Niseme ukweli kwamba, uongozi makini wa *TIF* umehakikisha kwamba, hawajipaki doa hilo pale walipoeneza miradi ya uchimbaji visima virefu na vifupi takribani mikoa yote ya Tanzania Bara.


Miradi hii ya visima ambayo *TIF* wameisambaza mpaka katika majengo ya kutolea huduma ya serikali ikiwemo shule za msingi, sekondari na zahanati inasimamiwa vema na kwa uadilifu mkubwa na Mkurugenzi wake Muhammad Aref Nahdi.


Katika eneo hili *TIF* wanaisaidia serikali kwa kugawa misaada katika maeneo mbalimbali yanayokumbwa na majanga hapa nchini kama vile matetemeko, mafuriko nakadhalika.


Wewe msomaji wangu ni shahidi mwaka 2016 *TIF* ilitoa msaada tani 132 za chakula pamoja na nguo, magodoro vyote vikiwa na thamani ya shilingi Milioni 252 kulipotokea tetemeko la ardhi mkoani Kagera.


Msaada huu ni mbali na ule *TIF* ilioutoa mwaka 2017 wa tani 41 za chakula Pemba visiwani Zanzibar wenye thamani ya shilingi Milioni 112 kufuatia mafuriko yaliyowaacha taabani wananchi wa huko.


Jambo la mwisho kwa leo nalotaka nikujuze ambalo labda *TIF* wenyewe hawalijui ni suala la *AJIRA* .


Tofauti na taasisi nyingine zisizo za kiserikali, hawa jamaa kwa ujumla wake wameisaidia mno serikali ya Rais Samia katika eneo la utoaji ajira.


Fikiria uwekezaji walioufanya kwenye Habari na Mawasiliano pekee ni vijana wangapi wamekamata ajira zinazosaidia mpaka familia zao huko waliko? Achilia mbali madereva na watendaji wengine wanaosaidia uendeshaji wa taasisi.


Kwenye eneo la elimu umeshajiuliza ni walimu wangapi waliokosa ajira serikalini na *TIF* imewapa ajira na maisha yanaendelea huku kipato chao kikisaidia kujenga uchumi wa familia zao na Taifa kwa ujumla?


Bado kwenye afya pamoja na shughuli za ujenzi wa vituo, madarasa, uchimbaji visima huko kote ajira zisizo rasmi zimekuwa zikiwasaidia watanzania kupunguza ukali wa maisha!


Nihitimishe makala haya kwa leo kwa kusema kuwa, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, wengi tumezoea kuwasema vibaya wenzetu waliojaribu kadiri ya uwezo wao kuisaidia jamii pale panapotokea mapungufu kidogo ya kibinadamu.


Lakini hatuko tayari kuwapongeza na kuwatia moyo wenzetu hao kwa yale mengi waliyopatia ambayo sisi wengine tumeshindwa hata kujaribu kuyafikiria.


Miaka 27 kwa kupima mafanikio ya taasisi kama *TIF* ni muda mfupi sana ukilinganisha na taasisi nyingine nchini ambazo leo zina miaka zaidi ya 50 lakini kwa kukosa viongozi madhubuti wenye nia njema na jamii, mafanikio yake tunayatafuta kwa tochi.


*Rashid Mtagaluka ni mwandishi wa habari na anapatikana kwa simu 0718406 242.*


No comments:

Post a Comment