NA. ELISANTE KINDULU, CHALINZE
DIWANI wa kata ya Bwilingu ,katika halmashauri ya Chalinze mkoa wa Pwani, Mh. Nassar Karama amesisitiza walimu kufanya kazi kwa bidii na kufuata kanuni za Utumishi wa umma ili kufikia malengo waliyojiwekea.
Mh. Nassar ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na walimu wa shule ya msingi Kibiki katika kata ya Bwilingu, alipowatembelea leo shuleni hapo.
Mh. Nassar amesema Jambo pekee linalomjengea mwalimu heshima ni pamoja uadilifu na ufanisi katika kazi yake ya ualimu vitakavyomfanya kuepuka migogoro na mwajiri wake.
Aidha Mh.Nassar amesema Kuwa kata yake bado inauhitaji mkubwa wa shule shikizi kutokana na wanafunzi wengi kusafiri umbali mrefu kufuata shule kongwe Mahali zilipo.
" Mfano Maeneo ya Kibiki Maziwa na Kitoho Kuna wimbi kubwa la wanafunzi kutembea umbali mrefu kuja kusoma hapa. Lazima tuone namna ya kuanzisha miradi ya Ujenzi wa shule kwenye maeneo yenye changamoto", alisema Diwani huyo.
Mh. Diwani aliuelekeza uongozi wa shule hiyo kuitisha vikao vya wazazi na wadau wa maendeleo ya elimu kwa ajili ya uhamasishaji wa kuwapatia watoto chakula shuleni, kuhimiza maadili pamoja na masuala ya kitaaluma.
Katika ziara hiyo walimu walitoa changamoto mbalimbali za kikazi zinazowakabili ikiwamo uhaba wa nyumba za walimu, uzio na kuwepo barabara inayopita pembezoni mwa eneo la shule ambayo jamii itakuwa ikiitumia badala ya barabara ya Sasa ambayo inapita katikati ya viwanja vya shule hiyo
No comments:
Post a Comment