Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo wamejengewa uelewa kuhusu Kanuni mbalimbali zinazosimamia Sekta ya Madini ili kuweka uelewa wa pamoja ikiwemo wizara kutoa taarifa kuhusu marekebisho yaliyofanywa kwenye Kanuni za Madini kuhusu Ushiriki wa Serikali kwenye Uchumi wa Madini.
Akitoa mada katika kikao hicho, Mwanasheria wa Wizara ya Madini Godfrey Nyamsenda amewaeleza wajumbe wa Kamati kuhusu Sheria zinazosimamia Sekta ya Madini na kuwaeleza kuwa ni pamoja na Sheria ya Madini, Sheria ya Baruti na Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta pamoja na Gesi Asilia pamoja na Sheria nyingine za Nchi.
Aidha, amefafanua kuwa, kulingana na matakwa ya Sheria ya Madini, shughuli za uchimbaji wa madini ya vito zinapaswa kufanywa na watanzania pekee isipokuwa pale wanapotaka kuingia ubia na asiye Mtanzania, Sheria inamtaka mbia kumiliki si zaidi ya hisa za asilimia 50 na mtanzania kubaki na umiliki wa hisa za asilimia 50 kwenye madini hayo baada ya kupata ridhaa ya Waziri wa Madini.
Vilevile, ameeleza kuhusu taratibu za kisheria zinazopaswa kuzingatiwa kuomba na kupewa leseni za Madini ikiwemo utafutaji, uchimbaji na biashara ya madini pamoja na utaratibu wa utengaji wa maeneo kwa ajili ya shughuli za uchimbaji mdogo wa madini nchini
Akizungumza katika kikao hicho, Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga amesema kutokana na wizara kuhamasisha uwekezaji, hadi sasa wizara imeweza kutoa leseni za uchimbaji mkubwa wa madini zipatazo 19 na kueleza kuwa, hadi kufikia mwaka 2025 miradi mikubwa ya madini ikiwemo ya Tembo Nickel, mgodi wa Nyanzaga na mingine itasaidia kuchangia maendeleo makubwa ya Sekta ya Madini.
Naye, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa akizungumza katika kikao hicho, amesema wizara itaendelea kufanyia kazi ushauri unaotolewa na Kamati. Ameongeza kuwa, wizara itaendelea kuweka mikakati ya kuiwezesha Sekta ya Madini kuchangia zaidi katika kuliingizia taifa fedha za kigeni ikiwemo kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa na kuongeza kwamba, hivi sasa sekta ya madini inachangia takribani asilimia 56 ya fedha za kigeni zinazotokana na mauzo ya bidhaa za madini nje ya nchi.
Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Simai Sadiki ameishukuru wizara kwa kutoa elimu hiyo kwa wajumbe wa kamati ambayo itawawezesha kuishauri wizara kikamilifu.