Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
limetenga kiasi cha shilingi bilioni 400 kwa ajili ya kazi ya kusambaza umeme
kwenye maeneo takribani 754 yaliyopitiwa na miundombinu ya umeme lakini hayana
umeme.
Hayo yalisemwa jana tarehe 24 Juni,
2019 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu wakati wa
Majumuisho ya Semina ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti
iliyohusu utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini
na mradi wa Kinyerezi 1 Extension (MW 185).
Semina hiyo ya siku moja ilihudhuriwa
na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati,
Dkt.Hamisi Mwinyimvua, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA),
Wakili Julius Kalolo, Menejimenti ya Wizara ya Nishati, REA na TANESCO.
“TANESCO imeshajipanga kufanya kazi
hiyo na Wizara inaendelea kusimamia kazi hizi za usambazaji umeme ili
kuhakikisha kuwa zinafanyika kwa ufanisi na tumeshafanya vikao mara kadhaa na
wadau wanaohusika na usambazaji umeme wakiwemo Mameneja wa TANESCO nchi nzima
lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata umeme.” Alisema Naibu
Waziri.
Aliongeza kuwa, katika mwaka wa Fedha
unaoanza mwezi wa Saba mwaka huu, kipaumbele kitakuwa ni usambazaji umeme
katika maeneo mbalimbali nchini kwani kila siku kuna ziada ya umeme ya kiasi
cha megawati 250 hadi 300 kwa siku.
Aidha kuhusu usambazaji umeme katika
Taasisi za umma kwenye miradi ya umeme vijijini alisema kuwa, Serikali kupitia REA
na TANESCO itaweka kipaumbele cha kupeleka umeme kwenye maeneo hayo ili uwepo
wa nishati kwenye vijiji hivyo uwe na tija.
Katika Semina hiyo, wajumbe hao
walielezwa mafanikio mbalimbali ya usambazaji umeme vijijini ambapo ilielezwa
kuwa, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Mei, 2019, jumla ya Vijiji 7,217 kati ya
Vijiji 12,268 ambayo ni asilimia 58.9 ya Vijiji vyote vimefikiwa na miundombinu
ya umeme.
Pia, hadi kufikia mwezi Juni 2020
jumla ya Vijiji 10,278 sawa na asilimia 84 ya Vijiji vyote vitakuwa vimepatiwa
umeme.
Kuhusu utekelezaji wa mradi wa
Kinyerezi I Extension (MW 185) ilielezwa kuwa, mradi huo utakamilika mwezi
Agosti mwaka huu na mkandarasi ni kampuni ya Jacobsen Electro ya Norway.
Katika Semina hayo, Wajumbe hao
walitoa maoni mbalimbali yatakayoboresha Sekta ya Nishati nchini ambayo Wizara
ya Nishati kupitia Taasisi zake iliahidi kuyafanyia kazi
No comments:
Post a Comment