Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Fedha na Utawala, Christopher
Bazivamo, akifungua Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati
la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ngazi ya wataalamu, Juni 3, 2019 jijini Arusha.
.............................................
Na Veronica Simba – Arusha
Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri
la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, umeanza leo Juni 3, 2019
jijini Arusha.
Akifungua Mkutano huo katika siku ya
kwanza katika mkutano huo ambao unahusisha ngazi ya wataalamu wa sekta husika, Naibu
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Fedha na
Utawala, Christopher Bazivamo, amewataka kujadili kwa uwazi changamoto
zinazokabili nchi wanachama hususan upatikanaji wa umeme wa uhakika ili
kuainisha mikakati ya kuzitatua.
“Jamii zetu bado hazijawa na umeme wa
uhakika ukilinganisha na sehemu nyingine za Dunia, hii ni changamoto ambayo tunahitaji
kuitafutia ufumbuzi, tujadili kwa uwazi ili tuone wapi tunakwama na namna gani
tutatue,” alisisitiza.
Akifafanua zaidi, Bazivamo alisema
changamoto za nishati kwa nchi za Afrika Mashariki zinahusisha mambo mbalimbali
ikiwemo nishati ya kupikia ambayo alieleza kuwa asilimia kubwa ya wanajamii wa
ukanda husika bado wanatumia kuni na mkaa; hali inayochangia uharibifu wa
mazingira.
Alisema haitoshi kuwaonesha wananchi
kuwa nishati ipo isipokuwa kuchukua hatua za kuifanya ipatikane kwao na kwa bei
wanayoweza kuimudu.
Aidha, Bazivamo amewashauri wataalamu
husika, kuhakikisha wakati wanahamasisha uwekezaji katika uzalishaji wa umeme,
wahamasishe pia uwekezaji katika usambazaji wa nishati hiyo ili kuwezesha hali
ya upatikanaji wake kwa jamii.
Pamoja na mambo mengine, Mkutano huo
wa 14 unatarajiwa kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa miradi na
program katika sekta ya nishati pamoja na maagizo yaliyotolewa katika Mkutano
wa 13 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati.
Aidha, Mkutano huo utapokea Rasimu ya
Makubaliano ya Awali (MoU) iliyoandaliwa na Sekritarieti ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki kuhusu Mradi wa Umeme wa Nsongezi katika Mto Kagera unaotarajiwa
kutekelezwa kwa ushirika wa nchi za Tanzania, Uganda na Rwanda ili ipitiwe na
nchi husika.
Mkutano ngazi ya Mawaziri utafanyika
Juni 7 mwaka huu, ambayo ndiyo siku ya mwisho ya mkutano husika.
Tanzania inawakilishwa na wataalamu
mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika
la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na taasisi mbalimbali zinazohusiana na
nishati kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Wajumbe wa Mkutano wa 14 wa Baraza la
Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ngazi ya
wataalamu, wakishiriki ufunguzi wa Mkutano huo Juni 3, 2019 jijini Arusha.
Wajumbe wa Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ngazi ya wataalamu, wakishiriki ufunguzi wa Mkutano huo Juni 3, 2019 jijini Arusha.
Wajumbe wa Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ngazi ya wataalamu, wakishiriki ufunguzi wa Mkutano huo Juni 3, 2019 jijini Arusha.
Wajumbe wa Mkutano wa 14 wa Baraza la
Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ngazi ya
wataalamu, wakishiriki ufunguzi wa Mkutano huo Juni 3, 2019 jijini Arusha.
No comments:
Post a Comment