Saturday, June 29, 2019

WAJAWAZITO WASHAURIWA KUACHA KUNYWA POMBE.

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

Kinamama wajawazito na wanaonyonyesha Manispaa ya Lindi Mkoani Lindi wameshauriwa kuacha kutumia vileo ikiwemo pombe na sigara ili kuepuka madhara ya kiafya ambayo yatamkuta mtoto atakae zaliwa.


Ushauri huo umetolewa na Veronica Mrope Muuguzi mkunga wa Kituo cha Afya cha Mji katika Manispaa hiyo leo alipokuwa anazungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG.


Mrope alisema Utumiaji wa vileo kwa akinamama wajawazito na wanaonyonyesha unapelekea watoto wanaozaliwa kuwa na utindio wa ubongo (watoto mataila) pamoja na tatizo la upumuaji.


Alisema hali hiyo inatokana na kemikali zilizokuwepo kwenye vileo hivyo, ambavyo vinamfikia moja kwamoja aliye tumboni kutoka kwa mama yake ama kwa njia ya kunyonyesha kutoka katika maziwa ya mama huyo.


Mrope alisema ili kuepuka madhara hayo na madhara mengine yanayoweza kumpata Mtoto aliye tumbuni ni vyema Mama Mjamzito akaacha kutumia aina hiyo ya vileo mpaka pale Mtoto wake atakapoacha kunyonya.


Nao baadhi ya Wahudumu wa Baa na Clab wa manispaa ya Lindi walidai kuwa kutokana na uzoefu wao katika mkoa huo wamama wajawazito kutumia pombe kali ni jambo la kawaida.


Mmoja wawahudumu hao ambae hakutaka kutaja jina lake alisema kuwa madhara ya pombe wanazokunywa kina Mama hao licha ya kuathiri mtoto kiafya lakini pia kunaweza kupeleke hata kutoka kwa ujauzito ama kujifungua kabla ya muda.


“Dada hawa wamama bora hata wangekuwa wanakunywa na kutoka lakini humu kwenye Bar yanayotoke ni mengi wakishalewa tuu pengine wanagombana na kupigana humu humu hivi ikitokea Mama huyo anapigwa tumboni unafikili kitatokea nini kwa mtoto huyo? Aliuliza muhudumu huyo.


Nae salma Abdull Mkazi wa Mpili pili manispaa ya Lindi Mkoani humo alisema anachukizwa na kitendo cha baadhi ya wanawake wanaonyonyesha kutumia vileo kwani vinaathili hata ukuaji wa mtoto.


Salma alidai kuwa wamama wengi wanaotumia pombe mara nyingi hupoteza hamu ya kula hivyo humfanya mtoto anaezaliwa na kunyonya kuwa dhoofu kwa kuwa amekosa chakula chenye vitamin kutoka kwa mama yake.


Dalini Athumani ni Mama mwenye Mtoto Mmoja na ni mkazi wa kata ya mikumbi katika Manispaa hiyo ya Lindi yeye alisema kuwa alikuwa analazimika kutumia Pombe wakati wa ujauzito wake kwa kuwa alisikia kutoka kwa Mashoga zake kuwa ukinywa Bia wakati wa ujauzito hautakuwa na tatizo la kupungukiwa na Damu.


“Mimi nilipokuwa na ujauzito wa huyu mwanangu nilikuwa nashindwa kunywa vile vidonge vyekundu vya kuongeza damu nilvyokuwa napatiwa Kliniki kwa sababu vilikuwa vinanichefua hivyo nikaona njia raisi ya kuongeza Damu ni kutumia pombe na kweli mpaka najifungua sikuwa na tatizo lolote la damu” Alieleza Dalini.


Watafiti wa mambo ya Afya wanasema kuwa, Pombe ni sumu kwa mtoto.


Tafiti zinaonyesha kuwa mama mjazito anapokunywa pombe inaingia moja kwa moja kwenye mzunguko wa damu wa mama kisha hufika kwa mtoto kwa kupitia kondo la nyuma (placenta).


Aidha, mara pombe inapoingia kwenye mzunguko wa damu wa mtoto, huathiri uwezo wa mtoto kupata chakula, virutubisho na oksijeni ya kutosha kwa ajili ya maendeleo ya kawaida katika ubongo na viungo vingine.


Tafiti hizo za kitaalamu katika mambo ya Afya zinaeleza kuwa hali hiyo inaweza kuathiri ubongo wa mtoto na ukuwaji wa viungo vya mwili kwa ujumla.


Uharibifu huo unaweza kuathiri uwezo wa mtoto kujifunza na kufikiri pindi anapozaliwa hali ambayo itajionesha kwa matendo yake kama mtoto na kama mtu mzima.


Aidha, utafiti umeonesha kwamba uwezo wa mimba kustahimili kiwango cha pombe ni mdogo mno hali ambayop huathiri ufanyikaji wa viungo na ukuwaji wake kwa kiasi kikubwa.


Baadhi ya madhara yanayoweza kumpata kiumbe aliye tumboni kwa mama kutokana na unywaji wa pombe kipindi cha ujauzito ni pamoja na

  • Kutoka/kuharibika kwa mimba
  • Mtoto kuzaliwa akiwa na uzito mdogo
  • Mtoto kuzaliwa akiwa na ulemavu wa mbavu na kidari (sternum)
  • Mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo ya mgongo uliopinda (kibiongo) na vidole vilivyoundana
  • Mtoto kuzaliwa akiwa na kichwa kidogo kuliko kawaida (microcephaly)
  • Mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo ya pua
  • Kuzaliwa na matatizo ya taya
  • Mtoto kuwa na matatizo ya kutokuona mbali
  • Matatizo ya moyo kama vile moyo kuwa na tundu
  • Matatizo ya figo
  • Mtoto kuwa na ubongo mdogo na pia matatizo ya akili
  • Mtoto kuzaliwa akiwa na mdomo sungura (lip palate na cleft palate)
  • Matatizo ya kimaumbile ya masikio na ulemavu kwenye sehemu za uzazi (genital malformations).

  • Aina mojawapo ya kansa ya chembe nyeupe za damu (Acute Myeloid Leukemia). Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa katika jarida moja la utafiti wa kansa la Marekani lijulikanalo kama Journal of the American Association for Cancer Research.

Aidha, utafiti huo umesema kuwa madhara hayo si ya muda bali ya kudumu ambayo yanaweza kusababisha kifo kwa mtoto, malezi na makuzi ya tabu na hata hisia mbalimbali katika maisha.

No comments:

Post a Comment