Imeelezwa kuwa, Mkandarasi wa mradi
wa umeme wa Rufiji, kampuni ya JV Arab Contractors na Elsewedy Electric ameanza
rasmi kazi za ujenzi wa mradi huo hapo jana tarehe 15/6/2019.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nishati,
Dkt Medard Kalemani tarehe mara baada ya kukagua kazi za maandalizi ya awali ya
ujenzi wa mradi huo akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina
Chonjo, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati
Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka na
watendaji wengine kutoka kampuni ya mkandarasi, Wizara ya Nishati na TANESCO.
Mkandarasi huyo anaanza ujenzi ikiwa
ni baada ya kufanya matayarisho mbalimbali ikiwemo upelekaji wa vifaa
vitakavyotumika ktk shughuli za ujenzi, uwepo wa kambi za wafanyakazi, Ofisi na
kukamilisha kazi nyingine za awali ambapo kwa mujibu wa mkataba, alipewa miezi
Sita ya kufanya kazi hizo ambayo ukomo wake ulikuwa ni tarehe 14/6/2019.
Dkt Kalemani alisema kuwa, kazi
anazoanza nazo ni upasuaji wa miamba ili kuruhusu maji kupita kwenda kwenye
mitambo ya kufua umeme.
Alisema kazi nyingine za awali
zitakazofanywa ni kujenga daraja la muda litakaloruhusu upitishaji wa vifaa
kwenda kwenye eneo jingine la kazi pamoja na ujenzi wa daraja la kudumu.
Dkt Kalemani alieleza kuwa,
Mkandarasi ameahidi kukamilisha mradi huo ifikapo mwezi Juni, mwaka 2022 na
mradi utatekelezwa kwa kasi na ikiwezekana, megawati zote 2115 zitapatikana kwa
wakati mmoja.
Kuhusu vifaa vitakavyotumika kwenye
mradi huo, Dkt Kalemani aliwataka kutumia vifaa vinavyopatikana nchini na kwa
vifaa visivyopatikana nchini, vitanunuliwa baada ya kupata kibali maalum.
Pia aliagiza Wataalam wa ndani kupewa
kipaumbele katika ujenzi wa mradi huo, ili waweze kusimamia mradi huo mara
baada ya mkandarasi kukamilisha kazi.
Aidha, aliwapongeza TANESCO na
TANROADS kwa kusimamia mradi huo ipasavyo, na kuwaagiza kuendelea kuwasimamia
wakandarasi usiku na mchana.
No comments:
Post a Comment