Monday, June 24, 2019

DIWANI WA TENGELEA, MKURANGA ATATUA TATIZO LA MAJI.

DIWANI wa kata ya Tengelea wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Shabani Manda amefanikiwa kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa eneo hilo kwa muda mrefu.


Akizungumza na wananchi wa eneo kata hiyo, Manda alisema walikuwa wakisubiri huduma hiyo kwa muda mrefu na kwamba sasa imefanikiwa kwa wananchi hao kupata huduma ya maji.


"Maji ni uhai maji ni maisha ya kila siku kwa mahitaji ya viumbe hai hivyo kupatikana kwa mradi huu mkubwa wa kisima utasaidia wananchi wa kata yangu kuondokana na changamoto hiyo. Alisema Manda.


Alisema Awali wananchi hao walikuwa wakipata tabu kubwa sana kutokana na kutumia visima vya kienyeji.


Aliongeza kuwa kutokana na changamoto hiyo kudumu kwa muda mrefu aliweza kupambana kutafuta wadau na kufanikiwa kuwapata wafadhili waliojitolea kujengea kisima kirefu katika msikiti wa Sunguni.


Aidha alisema kuwa Al Fridaus Charitable Foundation ndio taasisi iliyojitolea kuwajengea wananchi wa kata yangu kisima Chenye uwezo mkubwa wa kuhudumia wananchi wasiopungua 500.


Aliongeza kuwa maji hayo ni ya wananchi wote bila ubaguzi wa dini wala kabila hivyo kila mmoja yuko huru kutumia maji hayo.


Kwa upande wake kiongozi wa msikiti huo Hamisi Mohamed amempongeza diwani huyo kwa jinsi anavyojituma katika kutafuta wafadhili mbalimbali kwa lengo la kuendeleza kata ya Tengelea.


Aidha ameipongeza taasisi ya Al Firdaus Charitable Foundation kwa msaada wa kisima walichokitoa kwa wakazi wa eneo hilo kwani walikuwa na changamoto kubwa ya maandalizi kwa ajili ya kupata huduma ya kutawadha wakati wa kuswali.


Naye mwakilishi wa taasisi hiyo hapa nchini Buddy Amour amesema kuwa Taasisi yao imejikita katika kutatua changamoto mbalimbali kwa lengo la kuisaidia serikali kwani peke yake ni vigumu kumaliza changamoto za wananchi wake.


"Tumejipanga kama taasisi ili kuhakikisha tunawasaidia wananchi wa maeneo tofauti tofauti ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa wananchi wake popote pale walipo " Alisema Amour.


Aidha amewapongeza wakazi wa eneo hilo kwa jinsi walivyokuwa wakijitolea kwa lengo la ufanikishaji wa mradi bila ya malipo ya aina yeyote.


Aliongeza kuwa kwa wilaya ya Mkuranga wamekabidhi visima 10 katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kutokomeza uhaba wa maji katika maeneo mbalimbali na hivyo takribani ya wananchi wote watakuwa na huduma ya maji.

No comments:

Post a Comment