Tuesday, June 4, 2019

JELA MIAKA 30 KWA KUKUTWA NA BANGI.

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

MKAZI wa Kijiji cha Majengo, Kata na Tarafa ya Mtama, Wilaya ya Lindi, Ramadhani Haji Juma {23} amehukumiwa kwenda Gerezani kutumikia kifungo cha miaka {30}, baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na Madawa ya kulevya aina ya Bangi yenye uzito wa Kilo 7.8 kinyume cha Sheria.


Hukumu hiyo imetolewa juzi na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Lindi, Liliani Rugalabamo, baada ya Mshitakiwa kukiri kosa lililomkabiri bila ya kulazimishwa.


Baada ya Mshitakiwa kukiri kosa, Hakimu Rugalabamo alimuuliza mshitakiwa kama anazo sababu zitakazoishawishi Mahakama isimpe adhabu kali, ambapo Ramadhani Haji Juma aliomba asipewe adhabu kali, akidai ni mkosaji wa mara ya kwanza na alilazimika kujiingiza kwenye Biashara hiyo kwa lengo la kujipatia riziki ya kila siku.


“Mh. Hakimu naiomba Mahakama yako tukufu inisamehe na sitarudia kufanya kosa la aina hii tena kushiriki kazi hii ”Alisema Ramadhani.


Kufuatia utetezi huo, Hakimu Rugalabamo alirejea kwa Mwanasheria wa Serikali, Yahaya Gumbo iwapo anazo kumbukumbu za Makosa ya zamani kwa mshitakiwa na kujibu hana, huku akiiomba Mahakama impatie adhabu kali ili iwe fundisho kwake na wengine walio na tabia ya aina hiyo.


Hakimu Rugalabamo akimpatia mshitakiwa adhabu Stahiki katika kesi hiyo Namba 41/2019, alipinga utetezi huo kwa kusema hauna mashiko, kwani zipo njia nyingi za halali kama vile kuitumia Aridhi iliyopo kuzalisha Mali, yakiwemo Mazao ya Chakula na Biashara ili kuondokana na umasikini.


Akimpatia adhabu kwa mshitakiwa huyo kupitia kifungu cha 15 (A) kifungu kidogo cha kanuni ya kuzuia matumizi ya Madawa ya kulevya 2015 kilichofanyiwa Marejeo na Act 15/2017, Rugalabamo alimuhukumu kwenda Gerezani miaka (30).


Mwanzoni ilidaiwa Mahakamani hapo na Mwanasheria wa Serikali yahaya Gumbo, kuwa mshitakiwa alikamatwa eneo la Mitwero katika Manispaa ya Lindi na Askari WP 7203 D/C Kibibi, Mei 14 mwaka huu, kufuatia Gari namba T.540 DQJ alilokuwa akisafiria Mtuhumiwa huyo kufanyiwa ukaguzi.


Gumbo alidai kwamba katika ukaguzi huo, ndipo Askari Kibibi aliweza kubaini Madawa hayo ya kulevya aina ya Bangi yenye ujazo wa Kilo 7.8, yakiwa yamefungwa ndani ya mfuko wa Plastiki na kuwekwa kwenye Begi alilokuwa amewekea Nguo.

No comments:

Post a Comment