Monday, June 3, 2019

TFS BAGAMOYO YAKAMATA MKAA WA MAGENDO.

Wakala wa huduma za misitu nchini (TFS) wilaya ya Bagamoyo wamekamata mkaa magunia zaidi ya mia mbili yaliyokuwa yanapitishwa kwa njia za magendo.


Mkuu wa kikosi cha doria kutoka Wakala wa Huduma za Misitu TFS wilaya ya Bagamoyo, Yusuf Haruna amesema mkaa huo wameukamata kufuatia taarifa za wasamaria wema.


Amesema mkaa huo ulipakiwa kwenye Jahazi na kufichwa kwenye mkondo wa Bahari ya hindi unounganishwa na mto Ruvu wakisubiri kusafiri kuelekea Zanzibar.


Aliongeza kuwa, mara baada ya kupata taarifa hizo kikosi cha doria kilifika eneo la tukio ambapo kimekuta Jahazi hilo likiwa na mzigo huo huku mmiliki wa mkaa huo akiwa amekimbia.


Alisema utoroshaji wa mazao ya misitu ni makosa kwa mujibu wa sheria hivyo mzigo unaokamatwa unataifishwa kwa mujibu wa sheria huku chombo kilichobebwa hupigwa faini.


Akizungumzia hali ya utoroshaji wa mazao ya misitu kwa wilaya ya Bagamoyo, Mkuu huyo wa kikosi cha doria wilaya ya Bagamoyo, alisema bado kuna hali ya utoroshaji wa mazao ya misitu lakini kikosi chake kimejipanga kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa wilaya hiyo wandhibiti mianya yote inayotumika.


Na Meneja msadizi wa kanda maalum ya Saadan wilaya ya Bagamoyo, Hadija Msuya ametoa wito kwa wafanyabiashara wa mazao ya misitu katika wilayani humo kufuata sheria za uvunaji na usafirishaji wa mazao ya misitu.


Alisema ni vyema wafanyabiashara hao wakafuata sheria katika kuvuna na kusafirisha ili kuepuka usumbufu unaoweza kuwapata.


Alisema TFS wilaya ya Bagamoyo imejipanga kuhakikisha inadhibiti vitendo vyote vinavyokiuka sheria za uvunaji na usafirishaji wa mazao ya misitu.


Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano ili kubaini vitendo vya kiharifu ili kunusuru misitu katika wilaya hiyo.
    
Kikosi cha doria kutoka Wakala wa Huduma za Misitu TFS wilaya ya Bagamoyomara baada ya kukamata jahazi lililobeba mkaa na kufanikiwa kulifikisha bandari ya Bagamoyo na kutaifisha mkaa huku jahazi hilo likiwa chini ya ulinzi.

 

Jahazi likiwa limebeba mkaa wa magendo baada ya kukamatwa kama linavyoonekana likiwa katika bandari ya Bagamoyo.

No comments:

Post a Comment