Serikali imesema haina mpango wa
kuvibadili Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi kuwa VETA na badala yake imejikita
katika kuviboresha Vyuo hivyo kwa kuvikarabati na kuviongezea vifaa vya
kujifunzia na kufundishia ili viweze kutoa mafunzo bora zaidi.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni leo Juni
03, 2019 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha,
wakati akijibu swali la Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa (Rufiji), aliyetaka kujua
kama serikali haioni umuhimu wa kukibadili chuo cha Maendeleo ya Wananchi Ikwiriri FDC kuwa VETA ili kubadili
fikra za wananchi wa Rufiji, Kibiti na Ikwiriri na hatimaye kuleta mwamko wa
elimu.
Ole Nasha amesema serikali inaendelea
kuvikarabati vyuo hivyo ambapo awamu ya kwanza ya ukarabati unaohusisha vyuo 20
upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji na kwamba awamu ya pili inatarajiwa
kuanza mapema mwezi Juni, 2019.
Chuo cha Maendeleo ya Wananchi
Ikwiriri kilikuwa katika Awamu ya kwanza na ukarabati umekamilika.
Aidha katika mwaka wa fedha 2019/20
Rufiji ni miongoni mwa wilaya zilizotengewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo
cha Ufundi Stadi (VETA) cha Wilaya.
"Kwa sasa, Serikali haina mpango
wa kuvibadili Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi kuwa VETA na badala yake,
imejikita katika kuviboresha Vyuo hivyo kwa kuvikarabati na kuviongezea vifaa
vya kujifunzia na kufundishia viweze kutoa mafunzo bora" alisema Ole Nasha
Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi
vilianzishwa kwa lengo la kumsaidia mwananchi kukabiliana na changamoto za
kimaendeleo katika mazingira yake kwa kumpatia Maarifa na Stadi anuwai ambapo vyuo
hivi hutoa Elimu ya Ufundi Stadi katika hatua ya Kwanza hadi ya Tatu.
Mafunzo yanayotolewa katika vyuo
hivyo ni pamoja Ujasiriamali, Kilimo, Uvuvi, ufugaji na mengine kulingana na
mahitaji ya eneo husika na kwamba hivi sasa nchini kuna vyuo vya maendeleo ya
wananchi 55.
No comments:
Post a Comment