Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya ya Bagamoyo, Bi. Fatuma Latu amewaasa watumishi wa Halmashauri hiyo
kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni (STK) za utumishi wa
Umma ili kuleta matokeo chanya kwenye utumishi.
Bi. Fatuma Latu, ameyasema hayo
mapema wakati alipokuwa akifungua mkutano maalum wa watumishi takribani 200 wa
Halmashauri hiyo, uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri, katika kilele cha
maadhimisho ya juma la utumishi wa Umma.
“Kila mtumishi ahakikishe anafanya
kazi kwa kuzingatia Sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa Umma, hizi ziwe
dira wakati tukitimiza majukumu yetu ya kila siku ili kuleta matokeo chanya ya
utekelezaji wa shughuli za Serikali katika Halmashauri yetu” Alisema Bi. Fatuma
Latu.
Bi. Fatuma Latu pia ametumia fursa
hiyo kuwaasa Watumishi kuhakikisha wanajiepusha na vitendo vya rushwa, matumizi
ya lugha chafu, na kuhimiza ushirikiano baina ya watumishi katika ngazi zote,
huku akitanabaisha kwamba hatamvumilia mtumishi yeyote ambaye atapatikana na
makosa ya kuomba ama kupokea rushwa.
Akaongeza, Suala la kutunza siri pia
ni muhimu sana wakati wa utekelezaji wa Shughuli za Serikali kila mmoja katika
nafasi yake, utunzaji wa Siri unatufanya kufanya kazi kwa kuaminiana na kwa
usalama wakati wote hivyo kuongeza ari ya kutumikia Wananchi.
Vilevile, Mkurugenzi Mtendaji, Bi.
Fatuma Latu, amewakumbusha watumishi kuhakikisha wanapata chakula bora na
kujipa muda wa kupumzika baada ya kumaliza kutimiza majukumu yao ya kila siku
ili mwili uwe na Afya wakati wote na kuongeza uwezo wa kufanya kazi.
Nae, Mkuu wa Idara ya Utumishi na
Utawala Ndg. George Mwalukasa akizungumza na watumishi katika Mkutano huo
amewahimiza watumishi kuwa makini pale wanapotakiwa kuhuisha taarifa zao za
kiutumishi, kwani wengi wao wamekuwa na hulka ya kupuuzia maagizo ya usafishaji
taarifa za kiutumishi yanapotolewa, kwani kupuuzia usafishaji wa taarifa za
mtumishi kunaweza kupelekea mtumishi kuondolewa katika orodha ya malipo ya
mshahara.
Aliongeza kwa kusema “Mtumishi ambaye hatajaza fomu za OPRAS
kuaniza tarehe 01 Julai, 2019, ambapo OPRAS zitaanza kujazwa kwa njia ya
kielektroniki, hatapata mshahara hadi hapo atakapokuwa amejaza fomu hiyo ya
upimaji wa utendaji kazi wa Mtumishi, yaani OPRAS”.
Wakati huo huo, watumishi wamepata
darasa maalum la madhara ya kujihususha na vitendo vya rushwa ambapo Afisa
TAKUKURU – Elimu kwa Umma, Bi. Jane Mgaya amezungumzia mada maalum ya madhara
ya vitendo vya Rushwa katika utendaji kazi wa kila mtumishi anapokuwa
akitekeleza majukumu yake ya kila siku.
“Tuepuke mambo yanayopelekea uwepo wa
mazingira ya vitendo vya rushwa kutengenezwa, tunapokuwa tukitekeleza majukumu
yetu ya kila siku, mambo hayo ni pamoja na ukosekanaji wa uwazi katika
uwajibikaji, urasimu katika utoaji huduma na tamaa ya kujipatia mafanikio kwa
haraka” Alisema Bi. Jane Mgaya
Aliongeza, athari za rushwa ni kubwa
kwani rushwa huondoa utu na thamani ya mtu, hudhoofisha utoaji huduma bora,
kukosekana kwa uwazi na uwajibikaji katika utumishi wa umma na hupelekea
mtumishi kufanya maamuzi yenye upendeleo, hivyo akasisitiza kila mmoja
kushiriki katika vita dhidi ya rushwa ili kuiletea jamii yetu maendeleo kwani
vita dhidi ya rushwa si ya TAKUKURU peke yake bali ni ya jamii nzima ili
kuiletea jamii yetu maendeleo.
Wiki ya utumishi wa umma huadhimishwa
mara moja kila Mwaka kila ifikapo Mwezi Juni, ambapo shughuli mbalimbali za
kiutumishi huambatana na maadhimisho hayo, ikiwa na pamoja kusikiliza kero na
malalamiko toka kwa Watumishi na kuzipatia ufumbuzi,
Aidha, katika maadhimisho hayo
kunakuwa na semina mbalimbali zinazohamasisha weledi na utawala bora katika
utumishi wa umma, pamoja na mkutano maalum wa watumishi ambao hufanyika siku ya
kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma ambao huhudhuriwa pia na wadau mbali mbali
toka sekta binafsi zikiwemo taasisi za kifedha na mashirika binafsi Wilayani
hapa.
No comments:
Post a Comment