Monday, June 17, 2019

RAIS WA ZAMANI WA MISRI AFARIKI DUNIA.

Image may contain: 1 person, beard
Aliyekuwa rais wa Misri, Mohammed Morsi, ambae aliondolewa madarakani na jeshi mwaka 2013 amefariki dunia ghafla akiwa mahakamani.


Taarifa za kifo cha kiongozi huyo zimetangazwa na televisheni ya taifa hilo mara baada ya kifo hicho kutokea.


Mahakama nchini Misri ilibatilisha hukumu ya kifo mwaka 2016 dhidi ya rais huyo aliyepinduliwa.


Morsi alihukumiwa kifo baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na kutoroka kwa wafungwa wengi wakati wa mapinduzi ya mwaka 2011 nchini humo.


Alichaguliwa kuwa rais mwaka 2012 lakini akaondolewa katika mapinduzi ya kijeshi mwaka mmoja baadaye, kufuatia maandamano makubwa ya kupinga utawala wake.


Morsi alishahukumiwa kifungo cha maisha jela kwa mashtaka yanayohusu ugaidi.


Umauti umemkuta alipokuwa mahakamani akisikiliza mashtaka dhidi yake ya kujihusisha kijasusi na kundi la Hamas la nchini Palestina.


Kwa muda wote, Morsi na wafuasi wake wamekuwa wakishikilia msimamo kuwa mashtaka dhidi yake yamechochewa na uhasama wa kisiasa baina yake na uongozi uliopo kwa sasa.


Mtoto wa kiume wa Morsi, Abdullah hivi karibuni alilalamikia juu ya baba yake kunyimwa huduma muhimu za kiafya akiwa gerezani.


Aliliambia shirika la kimataifa la habari la AP mwezi Oktoba mwaka jana kuwa baba yake amekuwa akifungiwa muda mwingi kwenye selo ya peke yake na kunyimwa matibabu ya magonjwa yanayomsumbua ambayo ni shinikizo la damu na kisukari.

No comments:

Post a Comment