Monday, June 3, 2019

WANANCHI LINDI WASHAURIWA KUTUMIA KIFAA CHA UMETA ILI KUPATA NAFUU YA KUUNGANISHIWA UMEME.

NA HADIJA HASSANI, LINDI.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa Nishati vijijini Rea Mhandisi Amos Maganga amewashauri wananchi wa Mkoa wa Lindi kutumia kifaa cha umeme tayari UMETA Kuunganisha umeme katika Nyumba zao ili kuondokana na gharama za kuweka mfumo wa umeme.

Mhandisi Maganga ameyasema hayo leo Juni 03, 2019 mara baada ya kukagua Maendeleo ya Mradi wa usambazaji wa umeme vijijiji REA katika Wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi alipokuwa ameongozana na Wataalamu wa Bodi hiyo.

Maganga alisema huenda idadi ndogo ya wateja waliounganishwa kwa ajili ya kupata huduma ya Umeme inatokana na gharama kubwa ya kuweka mifumo ya umeme katika nyumba zao hivyo kupitia kifaa hicho wananchi wataweza kuunganishiwa huduma hiyo pasipo kuweka mifumo hiyo.

Alisema serikali kwa kutambua kuwa umeme huo wa Rea unaenda vijijini tena kwa wananchi walio wengi ilionelea kuwaletea kifaa hicho cha UMETA ili waweze kupata huduma hiyo ya Umeme kwa gharama nafuu zaidi.

Alisema vifaa hiyo vimetolewa 250 kwa kila mkoa ambavyo vinapaswa kuunganishwa bure kwa wateja wapya wa awali wa mradi huo wa Umeme vijijini.

Nae Msimamizi wa miradi ya Umeme Vijijini Wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi Lameck Njambo alisema kifaa hicho cha Umeme tayari UMETA hakina tofauti na mfumo wa kawaida wa umeme.
Alisema kifaa hicho huwa kina uwezo wa kuwasha taa, kutumia jiko la umeme, Tv, feni, friji pasi na vifaa vingine vya umeme kwa wakati mmoja.

Kwa mujibu wa Meneja wa Shirika la Umeme Tanesco Mkoa wa Lindi Felisian Makota alisema kuwa kati ya wateja 5000 wanaotarajiwa kuunganishiwa umeme kupitia Mradi huo wa umeme vijijini Rea ni wateja 290 Peke ndio waliounganishiwa kwa sasa.

No comments:

Post a Comment