Sunday, June 30, 2019

KLABU YA NGUMI KIWANGWA WAHITAJI MIL. 10

Na Omary Mngindo, Kiwangwa.

KLABU ya mchezo wa ngumi iliyopo Kiwangwa halmashauri ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, inahitaji kiasi cha sh. Mil. 10 ili iweze kuanzisha mradi.


Wakizungumza na Majira kijijini Kiwangwa, bondia Sabri Chips amesema kuwa, klabu yao inaendeleza mchezo huo kwenye mazingira magumu, kutokana na kukosa msada, hivyo kulazimika kuchangishana fedha zao kutoka mifukoni.


"Klabu yetu tumeshiriki michezo mingi ndani na nje ya nchi, lakini pamoja na ushiriki huo tunakabiliwa na ukosefu wa mtaji wa kujiendesha hali inayotufanya siku za mapambano ya nje ya Kiwangwa kulazimika kuombaomba kwa wadau," alisema Chips.


Kwa upande wake kocha Msaidizi Juma Gunta alisema kuwa wanahitaji fedha kiasi cha sh. Mil. 10 ili waweze kuanzisha mtaji wa biashara hatua itayowasaidia kuendeleza mchezo huo Kiwangwa, wilaya ya Bagamoyo Mkoa na nchi kwa ujumla.


"Tumeshiriki mapambano 36 ya ndani na nje ya nchi, katika michezo hiyo tumefanya vizuri katika nyanja ya nidhamu, pia katika michezo yetu wapiganaji mmojammoja kati ya kumi, sita tunashinda, wengine wanatoka sare," alisema Gunta.


Kocha huyo alisema kuwa katika mapambano ambayo wameshiriki kwa baadhi ya michezo waliyocheza hawajawahi kupigwa kwa Nock Out, na kueleza kuwa hiyo inatokana na ubora wa wapiganaji hao.


Nae Frielo Mgumba alisema kuwa wanapambana na hali zao kutokana na kuendesha klabu yao kwa kuchaangishana, huku wakimuomba Mbunge wao Ridhiwani Kikwete, diwani Malota Kwaga na wadau wengine wawatupie jicho katika kuuendeleza mchezo huo.


"Tunao viongozi wetu wenye uwezo wa kutusaidia katika kuendeleza mchezo wa ngumi ndani ya Kijiji chetu, halmashauri ya Chalinze, wilaya na Mkoa kwa ujumla tunawaomba watuangalie kwa jicho la pili," alisema Mgumba.

No comments:

Post a Comment