Monday, June 3, 2019

BODI YA NISHATI VIJIJINI YATAKA MKANDARASI KUONGEZA KASI YA KUSAMBAZA UMEME.

NA HADIJA HASSAN, LINDI


Bodi ya Wataalamu wa Nishati Vijijini (REA) imemtaka mkandarasi wa State Grid anaetekeleza Mradi wa Kusambaza umeme Vijijini kupitia Mpango wa Rea Mkoani Lindi kuongeza Magenge ya vijana ili kuharakisha Ukamilishaji wa Usambazaji wa Umeme Katika Mkoa huo.


Wito huo umetolewa na kaimu mwenyekiti wa Bodi hiyo Dk, Andrew Komba walipokuwa katika zihara ya siku mbili Mkoani humo kwa lengo la kukagua utekelezaji wa mpango wa usambazaji wa umeme vijijini.


Komba alisema pamoja na Bodi kuonyesha kuridhishwa na kazi zilizofanywa na mkandarasi huyo Mzawa lakini bado inamshauri kuongeza magenge ya vijana ili kazi iliyosalia iweze kumalizika kwa wakati.


Hata hivyo bodi ilimtaka mkandarasi huyo kuwa pamoja na kupeleka miundombinu hiyo ya umeme pia ahakikishe anaendelea kuunganisha huduma hiyo kwa wananchi.


Alisema ili azima ya Serikali ya kusambaza umeme vijijini iweze kukamilika inaenda sambamba na wananchi kuunganishiwa pamoja na kutumia huduma hiyo.


"hili lisiishie hapa tuu katika kupeleka miundombinu lengo kuu la Serikali kuleta huduma ya umeme Vijijini ilikuwa ni pamoja na kuhakikisha Wananchi wanaunganishiwa ili waweze kupata huduma hivyo malengo yenu mnayopanga kutekeleza yaendane na kusambaza umeme kwa wananchi" Alisema Dk, Komba.


Nae Kaimu Mkurugenzi mkuu wa Rea mhandisi Amosi Maganga alitumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi wa Mkoa huo ambao wamepitiwa na mradi wa umeme vijijini kuchangamkia fursa ya umeme waliyoipata kuunganisha umeme katika maeneo yao pamoja na kuanzisha shuguli ndogo ndogo za kiuchumi ili kuweza kujiongezea kipato.


Alisema Serikali tayari imeshatoa fedha za kutosha ili kutekeleza miradi hiyo ikiwa pamoja na kushusha gharama za uunganishwaji lengo likiwa kuwafikia wananchi wote katika maeneo yao tena kwa bei nafuu.


Nae mkurugenzi wa State Grid Charles Mlawa anaetekeleza Mradi huo wa usambazaji Umeme Vijijini Katika Mkoa wa Lindi aliihaidi Bodi hiyo kukamilisha kazi kabla ya mwezi desemba mwaka huu.


Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo wa Rea Meneja wa Shirika la umeme Tanesco Mkoa wa Lindi Felisian Makota alisema kuwa Mradi huo wa Rea hadi kukamilika kwake unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi Bilioni 20 za kitanzania sawa na Bilioni 4.7 kwa fedha za kimarekani na unatarajiwa kuunganishwa katika vijiji 133 vya Mkoa huo.


Aidha Makota pia alibainisha Wigo wa mradi huo ni kuunganisha 33kv Msongo wa kati wa umeme kwa km 392.350, 04/023kv Msongo mdogo wa Umeme 380,60km, 50kvA Mashine umba 185 Pamoja na 100KVA Mashine Umba 2, wateja wa laini moja 4708 na Wateja wa laini tatu 524 ambapo alieleza kuwa kazi hizo kwa sasa zimeshakamilia kwa Zaidi ya asilimia 40

No comments:

Post a Comment