Sunday, June 2, 2019

MADIWANI CHALINZE WAPEWA ELIMU

Diwani wa kata ya Mkange, Hussein Juma Hading'oka akichangia mada katika mafunzo hayo.
Afisa Mipango wa Halmashauri ya Chalinze, Shaabani Millao, akitwasilisha mada mbele ya madiwani wa Halmashauri hiyo.
.............................................


Na Omary Mngindo, Lugoba


MADIWANI wa Halmashauri ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wamepatiwa mafunzo maalumu ya namna ya kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao.


Mafunzo hayo ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI, kuhusu usimamiaji wa miradi, kupitia sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2016 kuingiza utaratibu huo kwa kifungu 64 (5) cha sheria hiyo ya mwaka 2016.


Madiwani wakiongozwa na Mwenyekiti Said Zikatimu, Makamu Juma Mpwimbwi na Mkurugenzi Amina Kiwanuka, wakufunzi wa mafunzo Shaabani Millao ofisa mipango wa halmashauri na Dkt. Daud Paschal kutoka Chuo Kikuu Mzumbe idara ya Uhasibu na fedha wametoa mada mbalimbali.


Akisoma mada katika kikao hicho, Millao amewaambia madiwani hao kwamba, ofisi hiyo kupitia sekretariet za mikoa na Mamlaka za mitaa imetekeleza kwa ufanisi mkubwa miradi ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya na shule za msingi na sekondari.


"Kifungu 64 (6) cha sheria hiyo kinatoa maana ya matumizi ya manunuzi ya umma ambayo ni utaratibu wa ushirikiano wa taasisi za umma kufanya ujenzi kwa kutumia wafanyajazi wake na mitambo yake yenyewe au kwa kushirikiana na taasisi za umma au nyingine binafsi," ilieleza sehemu ya taarifa ya Millao.


Imeongeza kwamba utaratibu huo umefafanuliwa katika sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2011, kanuni ya 167 ya ununuzi ya mwaka 2013 na sheria ya (marekebisho) ya 2016 kanuni ya 64 za ununuzi wa umma ya mwaka huo.


Taarifa ya Dkt. Paschal imegusia masuala ya fedha ambayo imewataka wanaosimamia miradi katika maeneo ya wananchi kuwajulisha wananchi fedha zinazoingia katika miradi yao, hatua itayowaongezea hamasa ya kujitoa kwenye utekelezaji wake.


"Fedha lazima zipokelewe kwa kukiri mapokezi ha kiadi kilichopokelewa, jamii husika ijulishwe kupitia mikutano kiasi kilichopokelewa, pia kuhimizwa wahusika kuchangia nguvu ili wajisikie kuwa wao ni wamiliki wa miradi," ilieleza taarifa ya Dkt. Paschal.


Kwa upande wao madiwani Ramadhani Mwinyikondo na Malota Kwaga wametaka mwongozo wa namna zinavyopatikana kamati za kusimamia miradi, na kujulishwa tofauti ya Mkandarasi na utaratibu mpya.


Rehema Mwene amegusia changamoto ya kuchelewa malipo ambapo mara kadhaa wamekuwa wakiambiwa kikwazo ni epika, hivyo wameomba washirikishwe kikamilifu ili wajionee sababu zinazochangia hali hiyo ya ucheleweshwaji wa malipo mbalimbali.


Kwa upande wake Zikatimu alisema kuwa utaratibu wa sasa wa manunuzi umekuwa mkombozi katika utekelezaji wa miradi ukilinganidha na hapo awali, ambapo miradi mingi ilikuwa inasuasua kutokana na mlolongo wa kumpata mkandarasi.

No comments:

Post a Comment