Tuesday, November 12, 2019

Wanaharakati washauri vyama vya siasa kuacha kujitoa...wadai huko ni kusiginwa kwa demokrasia nchini



Mwanaharakati huru Mackdeo Shilinde akizungumza jijini Dar es Salaam leo kuhusu kuwaomba vyama vilivyojitoa katika mchakato wa uchaguzi kurudi kuendelea na uchaguzi huo


Baadhi ya Waandishi wa habari.
Mwandishi wetu, Dar es Salaam

WANAHARAKATI wamewaomba vyama vya upinzani kurudi katika ulingo wa uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa wakisema kitendo chao cha kujitoa wanawakosesha haki wananchi kuchagua kiongozi wanayemtaka.

Hatua hiyo imekuja kufuatia vyama vikuu vya upinzani Tanzania kujitoa kwa madai ya wagombea wao kuondolewa na serikali pasipo na kuwa na sababu ya msingi.

Akizungumza na Bagamoyokwanza blog, Mwanaharakati wa Mambo ya kijamii, Mackdeo Shilinde, amesema vyama vya siasa vinapaswa kuwa mfano wa kuheshimu mamlaka lakini pia kuwapa haki viongozi wa chini yao ya kuendelea kuwani nafasi za uongozi.

Amesema sababu ambazo zimetajwa na vyama vya upinzani kuwa watu wao wameondolewa katika nafasi za kugombea kwa sababu nyepesi hazina mashiko kwa sababu tayari viongozi hao walishakata rufani zao na maamuzi juu ya hatma yao yalikuwa bado hayajatoka, kitendo cha kuwakataza ni kusigina siasa.

“Unajua vyama vya siasa vinatakiwa kuheshimu taratibu na sharia, kwa mujibu  wa kanuni za uchaguzi, wale wote ambao walionekana kuwa na dosari katika fomu zao walitakiwa kukata rufaa, na baadae wapewe hatma ya rufaa zao, na wagombea wengi walifanya hivyo lakini kabla ya rufaa hizo kusikilizwa vyama vimekimbilia kujitoa na kuhatarisha nafasi za watu kugombea huu ni unyama” alisema.



Amewashauri Viongozi wa vyama vya upinzani kurudi tena wakatafakari na wagombea wao, wakawashirikishe waseme je ni kweli wagombea wao hawataki kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mtaa? lakini vilevile vyama vya upinzani wakafate taratibu wa katiba yao




Hata hivyo Mwanaharakati wa mambo ya kijamii kutoka taasisi isiyo ya kiserikali ya Alliance for Development (ADO), Ally Mwinyi amesema kuwa wagombea wa vyama vya upinzani wanaojiondoa kugombea katika uchaguzi wa serikali za mtaa wanadhoofisha afya ya demokrasia nchini na kuwanyima wananchi demokrasia ya kuchagua kiongozi wanaye mtaka.




"Jambo hili la kujitoa kwenye uchaguzi wa serikali za mtaa si jambo zuri kwa afya ya Demokrasia na ni kuwanyima wananchi demokrasia ndani ya demokrasia"




Mwinyi amesema kuwa demokrasia ni kuwa tayari kufata zile hatua zote za uchaguzi kwa sababu zisipofatwa ni kuharibu kanuni na taratibu zilizowekwa kwaajili ya afya ya Demokrasia.




Hata hivyo Mwinyi amesema kuwa kitendo cha baadhi ya vyama vya siasa kutoa tamko kabla  ya majibu ya rufaa zao hayajatoka hii si picha nzuri kwani vyama hivyo kwani vinasigina demokrasia.




"Sisi kama wanaharakati tunachopenda kutoa rai yetu kwa vyama viheshimu demokrasia, vionyeshe kuwa wao ndio wa kwanza wa kuonyesha afya ya demokrasia".




Mwinyi amesema kuwa watanzania wanahitaji watu kwaajili ya kuwatetea pamoja na kuwaongoza na hakuna njia nyingine isipokuwa ni kufanya uchaguzi kwa kufata taratiu zilizowekwa.


No comments:

Post a Comment