Thursday, November 14, 2019

MASHUJAA FM LINDI WAKABIDHI VIFAA VYA KUHIFADHIA TAKA KWA DC WA LINDI.

 
Meneja wa Mashujaa FM Mkoa wa Lindi zakia Mdemu (kulia) akimkabidhi Mkuu wa wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga vifaa vya kuhifadhia taka katika hatua ya kuunga mkono juhudi za serikali za usafi wa mazingira.
.............................................

Na Hadija Hassan, Lindi.

Kampuni ya mashujaa group kupitia kituo chao cha radio cha mashujaa FM mkoa wa Lindi imekabidhi vifaa vya kuwekea taka vyenye thamani ya Shilingi milioni 1.2 kwa Manispaa ya Lindi Mkoani humo.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo meneja wa Mashujaa FM Mkoa wa Lindi zakia Mdemu alisema kuwa lengo la kutoa vifaa hivyo ni kutaka kuunga mkono jitihada zinazofanywa na viongozi wa Mkoa huo za kufanya mji huo kuwa msafi.

Zakia alisema wao kama Mashujaa FM moja ya matamanio yao ni kuona Manispaa ya Lindi kuwa ni miongoni mwa Manispaa na Wilaya zinazoongoza kwa usafi hapa nchini.

Alisema ili kutimiza azma hiyo Kampuni yao pamoja na kutoa vifaa hivyo vya kuhifadhia taka imejikita katika kuelimisha jamii juu ya masuala ya usafi wa mazingira katika maeneo yao.

Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, Mkuu wa wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga aliushukuru uongozi wa Mashujaa FM kwa kukubali ombi lao la kusaidia vifaa hivyo ambavyo vitakuwa chachu ya kuendeleza usafi wa Manispaa hiyo.

Alisema moja ya changamoto kubwa inayoikabili Manispaa hiyo ni kukosa vifaa maalumu vya kuhifadhia taka kwenye barabara za mitaa ambapo kwa kiasi kikubwa inachangia taka zinazozalishwa na watembea kwa miguu kuzagaa katika mitaa jambo ambalo licha ya kuwa ni hatari kwa afya za wananchi, lakini pia halileti taswira nzuri ya mji.

Hata hivyo Ndemanga alisema kuwa vifaa hivyo vitawekwa katika maeneo ya wazi hasa maeneo ya sokoni, vituo vya mabasi na Hospitali ambapo kunamsongamano mkubwa wa watu ili taka watakazokuwa wanazizalisha waweze kuziweka katika vifaa hivyo.

Nae Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi Jomary Satura alisema kuwa vifaa hivyo vitaenda kupunguza changamoto ya uwepo wa vifaa vya kuhifadhia taka kwenye mitaa ambapo kwa sasa mahitaji ni 200 na zilizopo ni 38.

Hata hivyo Stura alitoa wito kwa Taasisi zingine zilizopo katika Manispaa hiyo kuunga mkono jitihada za kuweka mji safi zinazofanywa na Manispaa pamoja na Mkoa kwa ujumla kwa kununua vifaa mbali mbali vifaa vya kuhifadhia taka na vifaa vingine vya usafi wa mazingira.
 
Sehemu ya vifaa hivyo vya kuhifadhia taka vilivyotolewa na Kampuni ya mashujaa group kupitia kituo chao cha radio cha mashujaa FM mkoa wa Lindi kama vinavyoonekana katika picha.

PICHA ZOTE NA HADIJA HASSAN. 

No comments:

Post a Comment