Friday, November 15, 2019

WANANCHI KISARAWE WAFURAHIA ELIMU YA KODI TOKA TRA.

Na Shushu Joel.

WANANCHI wa wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani wamefurahishwa na huduma ya elimu kwa mlipa kodi inayotolewa na mamlaka ya mapato nchini (TRA).

Wakizungumza mara baada ya kutembelewa na wahudumu kutoka TRA walisema kuwa elimu imekuwa kubwa na yenye mashiko kwa wafanyabiashara.

James Joackim ni mmoja wa wafanyabiashara wa muda mrefu katika wilaya hiyo anasema kuwa tangu aanze biashara kipindi hiki amefurahishwa na huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo kwa jinsi wanavyojitoa kuwaelimisha wafanyabiasha.

"Miaka ya nyuma ilikuwa ukiwaona watu kutoka TRA unakuwa kama umewaona polisi hata ilifikia hatua ya kuwaona watu wa mapato unafunga duka lakini kipindi hiki ni raha sana"Alisema Joackim.

Aidha aliongeza kuwa elimu hii iendelee kutolewa mara kwa mara ili wafanyabiasha waweze kupata elimu zaidi.

Kwa upande wake Bi' Mariam Mbaga ameishukuru mamlaka ya mapato kwa kuelimisha juu ya utoaji wa risiti kwa wateja.

Pia amesema kuwa amewataka wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi katika zoezi linalofanywa na mamlaka ya mapato kwani elimu ni nzuri sana hivyo ukikosa elimu hii utajutia sana.

Naye Mkurugenzi wa huduma ya elimu kwa walipa kodi Richard Kayombo alisema kuwa mamalaka ya mapato nchini imeamua kuwafuata wananchi katika mkoa wa Pwani na Morogoro kwa madhumuni ya kuwaelimisha na kuwasaidia kutatua changamoto zao.

"Kampeni hii ya kuwaelimisha wananchi juu ya ulipaji wa kodi kwa hiyari ni endelevu na litafika kila mkoa kwa lengo la kuwasaidia wafanyabiashara na wananchi juu ya malipo ya kodi" Alisema Kayombo.

Aliongeza kuwa sio kila mtu anatakiwa alipe kodi hivyo ni muhimu sana kuwasikiliza watoa huduma kutoka TRA ili waweze kukuelimisha juu ya nani anastahili kulipa au kutokulipa.

Aidha Kayombo aliongeza kuwa dhamira ya mamlaka ni kuwaelimisha wananchi juu ya upataji wa namba ya utambulisho kwa mlipa kodi (TIN) na uchukuaji wa risiti kwa wanunuzi ni jambo la muhimu sana.

Akitoa ufafanuzi juu ya faida za kulipa kodi mkurugenzi huyo wa huduma ya elimu kwa walipa kodi alisema kuwa miradi yote inayotekelezwa kwa pesa za ndani ni matokeo ya ulipaji kodi.

Amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la ulipaji kodi za majengo, biashara na kodi zjngine ili kuisaidia serikali katika ufanikishaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wingi.

No comments:

Post a Comment