Thursday, November 7, 2019

KITUO CHA AFYA CHALINZE CHAZIDIWA NA WAGONJWA

 
Mkurugenzi wa shule ya Chalinze Modern Islamic, Omari Swed, akimkabidhi Mganga Mfawidhi wa kituo hicho Dkt. Sud Msakamali,kiroba cha sabuni ya unga, kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete.
........................................
Na Omary Mngindo.


Kituo cha afya Chalinze wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, kinakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa majengo sanjali na msongamano wa wagonjwa.


Kituo hicho kilichoanza kama zahanati mwaka 1982 kabla ya kupandishwa hadhi mwaka 1996 kuwa kituo cha afya, majengo yake yamekuwa chakavu huku baadhi yake hayana linta hatua ambayo ni hatari kwa usalama.


Hayo yamebainishwa na Mganga Mfawidhi wa kituo hicho Dkt. Sud Msakamali, akizungumza na Waandishi muda mfupi baada ya shule ya Chalinze Modern Islamic kufanya usafi pamoja na kukabidhi sabuni kwa uongozi wa Kituo.


Mbele ya Mkurugenzi wa shule ya Chalinze Modern Islamic, Omari Swed na Mbunge wa Jimbo hilo Ridhiwani Rikwete, Msakamali alisema kuwa kituo hicho kinapokea wagonjwa 300 kwa siku, huku kikizalisha watoto kati 130 mpaka 150 kwa mwezi.


"Kubwa la kwanza ni kuboreshwa miundombinu ya majengo, sababu wateja wanaokuja ni wengi, idadi ya majengo ni ndogo hivyo kusababisha foleni na msongamano, pia kutokwepo uzio ni changamoto kubwa watu wanapita muda wote," alisema Dkt. Msakamali.


Akizungumzia changamoto hiyo, Ridhiwani aliipongeza shule ya Chalinze Modern Islamic, kwa namna wanavyojitoa katika kufanikisha maendeleo, huku akishukuru msaada wa mifuko kumi ya saruji na karatasi za mitihani rimu 15 kwenye shule ya msingi ya Kibiki.


Aidha amewapongeza madaktari na watumishi wa Kituo hicho, huku akisema kuwa serikali imeshaanza kuzitafutia ufumbuzi, na kwamba TACAIDS imeshaanza ujenzi wa maabara itayojihusisha na upimaji wa vipimo vyote ikiwemo ya damu.


"Kama mnavyotambua, vipimo vya binadamu kwa magonjwa yote yanategemea upimaji wa damu, hilo limepewa kipaumbele, pia tunajenga chumba cha dharula kitakachosaidia wagonjwa watakaokuwa wanafika kwa ajili ya matibabu," alisema Ridhiwani.


Awali Mkurugenzi wa shule ya Chalinze Modern Islamic, Omari Swed akizungumza baada ya zoezi la usafi na kukabidhi sabuni za maji chupa 10, miche 15 ya sabuni ya kufulia na kiroba cha sabuni ya unga, alisema kuwa shule imejitoa kwa hali na mali kusaidia shighuli za kimaendeleo.


"Shule yetu ya Chalinze imekuwa mstari wa mbele kusaidia shughuli za kimaendeleo katika nyanja tofaiti, juzi tulikwenda shule ya msingi ya Kibiki tumesaidia mifuko kumi ya saruji na rimu 15 za karatasi kwa ajili ya mitihani," alisema Swed.

No comments:

Post a Comment