Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela akitoa neno wakati wa kufunga Tamasha la Urithi Wetu leo jijini Mwanza |
Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Mwanza.
Serikali imewataka waandaaji wa Tamasha la Urithi Wetu kuwa wabunifu kwa
kuongeza michezo mbalimbali ya jadi ambayo itasaidia kukuza kazi za sanaa na
utamaduni wa Mtanzania ili kukuza fursa za utalii na kuwaongezea wananchi
kipato.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mali Asili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala
leo jijini Mwanza wakati wa kufunga Tamasha la Urithi Wetu kwa naiaba ya Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa.
“Nimepita kila mabanda, wananchi wamepata fursa ya kutangaza kazi zao
mbalimbali za kiuchumi zinazowasaidia kukuza kipato chao na uchumi wa taifa kwa
ujumla. Rais Dkt. John Pombe Magufuli yupo mstari wa mbele katika kuinua na
kusimamia utamaduni wetu” alisema Dkt. Hamis Kigwangala.
Dkt. Kigwangala amesisistiza kuwa Tanzania inafursa nyingi za
kiutamaduni ambapo amebainisha kuwa ni nchi pekee barani Afrika inayojumuisha
zaidi ya makabila 128 ambayo yapo kwenye makundi makuu manne ya makabila yanayopatikana
Afrika yanayojulikana kama Wakushi, Khoisan, Wabantu na Waniloti.
Aidha, Dkt. Kigwangala alibainisha kuwa tamasha la urithi wetu lina
lengo la kuendeleza falsafa ya nchi yetu ambayo Baba wa taifa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kulinda utamaduni wa
Mtanzania.
Ili kulifaya tamasha la urithi liwe endelevu, Dkt. Kigwangala amesema
kuwa ni lazima wananchi wawe na furaha ambapo tamasha hilo linaongeza hamasa
katika michezo, sanaa na utamaduni hatua itakayowapelekea wananchi wawe wabunifu,
wenye furaha na wenye mawazo mazuri yanayowashirikisha wadau wote wa maendeleo
ikiwemo sekta binafsi.
Naye Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison
Mwakyembe amesema kuwa Watanzania wanahaki ya kumshukuru Baba wa Taifa Mwl.
Julius Nyerere ambapo mara baada ya kupata uhuru Desemba 9, 1961 alikuwa mstari
wa mbele katika kusimamia utamaduni wa Mtanzania.
Akinukuu maneno ya Baba wa Taifa Mwl. Nyerere Waziri Dkt. Mwakyembe
alisema “‘Taifa lisilo na utamaduni wake, ni taifa mfu.’ Watanzania tumeamka,
tamasha hili linatukumbusha tujitambue sisi ni akina nani. Namshukuru Mungu
tumejitambua ndio maana nawashukuru wana Mwanza, wizara zetu za Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Mali Asili na Utalii kwa kurejesha na
kusimamia tamasha hili linalotukumbusha sisi ni ni Watanzania, tujivunie
Uafrika wetu.”
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela amesisitiza kuwa Mwanza
ndio kitovu cha nchi za maziwa makuu ambapo kuna mfanano wa mambo ya kijiografia
yanayoifanya Mwanza kuwa katikati ya nchi za Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki.
Hii ni sifa inayoifanya mkoa huo kuendelea kuwa mwenyeji wa tamasha la utithi
wetu.
Jiografia hiyo inaipa mwanza nafasi kubwa zaidi ambayo itatoa fursa
kwa nchi zote za Afrika mashariki kushiriki katika tamasha hili kwa ufanisi
zaidi ambapo Mkuu huyo wa mkoa amewahakikishia washiriki wote ulinzi na usalama
wakati wa tamashaha hilo mwakani 2020 ambalo litafanyikia tena jijini Mwanza.
Tamasha la Urithi wetu lilianza Oktoba 31 na kuhitimishwa Novemba 02 ambapo
liliongozwa na kauli mbiu “Urithi wetu, Fahari yetu. Tamasha hilo lilpambwa na
kushereheshwa kwa michezo mbalimbali ikiwemo ngoma za asili, kwaya, mbio za
baiskeli, mbio za mitumbwi pamoja na mchezo wa bao.
No comments:
Post a Comment