Tuesday, November 19, 2019

Diamond Platnumz atunukiwa tuzo ya kujali na kuthamini jamii..wasema anastahili kupewa hongera na kutiwa moyo




Taasisis ya The Foundation for Conserving Natural Resources Based for Future Generation (FCRFG) na wadau wengine wametangaza nia yao ya kumtuza msanii maarufu hapa nchini Nasib Abdul maarufu Diamond Platnumz tuzo maalum ikiwa ni sehemu ya kutambua jitihada zake anazozifanya katika jamii.

Diamond ameweza kujitoa na kusaidia jamii kwa njia tofauti, ameweza kuwalipia watoto gharama za upasuaji wa moyo katika hospitali ya Taifa Muhimbili, kufuturisha watu wa makundi maalum, kutoa michango ya madawati, kutoa bodaboda kwa vijana na kusaidia wakina mama wajasiliamali.

Akizungumza na wanahabari mapema hii leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya TCRFG Bw. Omary Kalekela amesema wameamua kufikia maamuzi hayo baada ya kutafakali kwa kina kazi anazofanya msanii huyo kwa jamii.

“sisi kama wadau wa maendeleo tumeona msanii huyu amefanya mengi mazuri lakini kubwa ambalo limetugusa ni suala la kujitolea kuwalipia watoto wenye matatizo ya moyo pale hospitali ya taifa ya Muhimbili, ni kitendo ambacho kinatia moyo na faraja kwa jamii, kukaa kimya bila kumpa pongezi na kumtia moyo itakuwa si uungwana na ni uchoyo wa fadhila, sisi kama wadau wa maendeleo hatupo tayari kuwa wachoyo wa fadhila” alisema Kalekela.

Alisema tuzo hiyo inatarajiwa kutolewa katika ofisi za wasafi media, Jumamosi hii, pia siku hiyo Diamond Platnumz atavalisha joho maalum na kukabidhiwa Jogooo ikiwa ni ishara ya ujemedari wake wa kufanya kazi bila kuchoka licha ya kwamba hakusoma na kufikia ngazi ya digrii.

Pia Taasisi hiyo ilitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujitoa kwake na kuwathamini wasanii hadi kufikia hatua ya kutoa milioni 100 kwa ajili yao, lakini pia amesema wataendelea kumuombea Rais na wasaidizi wake wawe na afya njema na waendelee kutekeleza majukumu yao wakiwa na afya njema.

No comments:

Post a Comment