Friday, November 1, 2019

WENYE MASHAMBA PORI KIBAHA WAPEWA MIEZI MIWILI.

Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya mji Kibaha wakiwa katika kikao cha kujadili mambo mbali mbali ya maendeleo ikiwemo kuweka msimamo juu ya kuyataifisha maeneo yote ambayo yamegeuka kuwa mashamba pori.

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani nje ya ukumbi wa mikutano katika halmashauri ya mji kibaha akizungumzia kuhusina na msimamo wake pamoja na madiwani juuu ya kuyataifisha maeneo ambayo watu wake wamehindwa kuyaendeleza.

Madiwani wa halmashauri ya mji Kibaha wakiwa katika kikao cha baraza hilo kwa ajili ya kujadili changamoto mbali mbali zilizopo katika sekta mbali mbali pamoja na kuweka mipango mikakati ambayo itasaidia kuwaletea maendeleo wananchi.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji Kibaha Jenipher Omolo akielezea jambo kwa waandishi wa habari kuhusina na mikakati ambayo wameiweka katika kukabiliana na  changamoto ya kuwepo kwa mashamba pori ambayo yamekuwa ni kero kwa kipindi kirefu.

Mwenyekiti wa halmashauri ya mji Kibaha Leornad Mlowe akifafanua jambo kwa waandishi wa habari hawapo picha kuhusiana na maazimio waliyoyafikia katika kikao cha baraza la madiwani kuhusiana na chanagamoto ya kukithiri kwa mashamba pori na kuyataifisha kwa yale maeneo ambayo hayaendelezwi,(PICHA ZOTE NA VICTOR MASANGU).
...................................................


VICTOR MASANGU, KIBAHA

BARAZA la madiwani katika  halmashauri ya mji Kibaha mkoani Pwani limeazimia kwa pamoja kuyataifisha maeneo yote ambayo yametelekezwa kwa kipindi kirefu bila ya kuendelezwa na kupelekea kuwa mashamba pori ndani ya kipindi cha miezi miwili endapo bado yataonekana  hayajaendelezwa.

Kauli hiyo ilitolewa  na Mwenyekiti wa halmashauri ya mji Kibaha Leornad Mlowe kwa niaba ya baraza la madiwani  ambapo amebainisha kuwa tatizo hilo limekuwa sugu kwa kipindi cha  muda mrefu hivyo wamechoshwa na hali hiyo, ambapo wataandika barua rasmi kwa Waziri mwenye dhamana ili sheria na taratibu ziweweze kuchukua mkondo wake ikiwemo pamoja na  kufuta kabisa  hati za wamiliki wa maeneo hayo.

“Sisi kama baraza la madiwani la halmashauri ya mji kibaha baada ya kukaa kikao chetu cha kawaida tumeweza kujadili mambo mbali mbali ya maendeleo lakini kubwa zaidi tumeamua na kukubaliana kwa pamoja ni kutaifisha maeneo yote ambayo hayajaendelezwa kwa kipindi kirefu na sisi tumetoa muda wa miezi miwili kwa wahusika kuyaendeleza mtu ambaye atakaidi basi hatua zitachukuliwa kwani hii hali imekuwa ni tatizo na lengo letu ni kuleta maendeleo kwa wananchi,”alisema Mlowe.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya Kibaha mji Jenipher Omolo alikiri  kuwepo kwa baadhi ya watu wanaomiliki mashamba makubwa bila ya kuyaendeleza kwa miaka zaidi ya mitatu kinyume kabisa na sheria na taratibu za ardhi  hivyo kusababisha  ukosefu mkubwa wa mapato na kuzorotesha kasi ya maendeleo kwa wananchi kutokana na baadhi ya  maeneo hayo kuwa mapori makubwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama ambaye ndiye aliwasilisha hoja yake  binafsi katika kikao  cha baraza la madiwani kuhusiana na kukithiri kwa maeneo mengi kuwa mapori amebainisha kuwa nia ya serikali ya awamu ya tano ni kuwa na Tanzania ya viwanda hivyo watu wote walioyatelekeza maeneo yao yatarudishwa kwa serikali na kubadilishiwa matumizi mengine.

Mshama aliongeza kuwa  katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Kibaha kuna changamoto kubwa ya kuwepo kwa maeneo ambayo yamegeuka kuwa mashamba pori kutokana na wahusika kutoyaendeleza kabisa hivyo kwa sasa atahakikisha anashirikiana bega kwa bega na madiwani pamoja na mamlaka zinazohusika ili kuweza kuyarudisha maeneo hayo kwa serikali yaweze kutumika kwa shughuli nyingine za kimaendeleo.


“Kwa kweli ndugu waandishi ili tatizo la kuwepo kwa mashamba pori katika mji wetu wa kibaha limekuwa ni la miaka mingi sana na tayari nilishawaambia kuwa maeneo yote ambayo yamechukuliwa ni lazima yaendelezwa na sio kuyaacha kwa miaka mingi bila ya kuyafanyia kitu chohote lakini kuna baadhi ya watu bado wamekuwa ni wagumu na lengo letu kubwa ni kuona mji wetu una kuwa ni sehemu ambayo sio mapori kama ilivyo kwa sasa,”alisema Mshama.

Kumekuwepo na wimbi la baadhi ya maeneo katika Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani ambayo hayajaendelezwa kwa kipindi cha miaka mingi hivyo kupelekea kugeuka kubwa mashamba pori na  mengine kuwa vichaka vikubwa ambavyo vimekuwa ni  sehemu ya wahalifu kwenda kujificha pindi wanapofanya matukio mbali mbali ya uporaji.

No comments:

Post a Comment