Na
Omary Mngindo, Mkuranga
VIJIJI
takribani 12,319 vinataraji kufikiwa na huduma ya umeme ifikapo mwaka 2021,
ikiwa ni dhamira ya Rais Dkt. John Magufuli ya kuhakikisha vijiji hivyo
vinakuwa na Nishati hiyo.
Naibu
Waziri wa Nishati Subira Mgalu aliyasema hayo wilayani Mkuranga, katika Mkutano
Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), uliozungumzia utekelezaji wa Ilani, huku
Katibu wa NEC (Siasa na Uhusiano wa Kimataifa) Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga
alikuwa mgeni rasmi.
Alisema
kuwa dhamira ya Rais John Magufuli ya kutaka vijiji vyote vinakuwa na umeme
ifikapo Juni 2021, Wizara yake chini ya Waziri Dkt. Medard Kalemani wanaitekeleza
kikamilifu, na kwamba wana matumaini mpaka ifikapo 2020 watakuwa wametimiza
adhima hiyo.
Aliongeza
kuwa kazi ya uunganishaji umeme vijijini inaendelea vizuri, na kwamba kwa
Wilaya ya Mkuranga tayari vijiji vipya 36 vimeunganishiwa Nishati hiyo katika
kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya tano, iliyoingia madarakani
Oktoba 2015.
"Oktoba
2015 wakati Serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani, kulikuwa na vijiji
20 tu vilivyokuwa vimeunganishwa na umeme hapa Mkuranga, kutokana na kasi
iliyopo, sasa tumeongeza vijiji vingine 36 na kazi inaendelea," alisema
Mgalu.
Aidha
Mgalu amempongeza Mbunge wa Mkuranga (Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi) Alhaj
Abdallah Ulega kwa kazi anayondelea kuifanya, huku akisema kwamba kupitia ziara
zake za kuwasha umeme, akiwa na Ulega wananchi takribani 1,200 wameunganishwa.
Akizungumzia
sekta ya gesi, Naibu Waziri huyo alisema kuwa kwa kipindi hiki cha 2019 viwanda
takribani 50 vimeshaunganishiwa Nishari hiyo, huku akieleza kuwa ni hatua nzuri
na ya kujivunia katika kipindi cha miaka minne ya Rais Magufuli.
Kwa
upande wake, Mbunge Ulega ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Nishati, kwa
kazi kubwa inayoendelea kufanyika ya kuhakikisha wa-Tanzania wote wanafikiwa na
umeme pasipo kubagua.
No comments:
Post a Comment