Na Jovina Bujulu,
MAELEZO, Dar es Salaam
Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli imeendelea kujidhihirisha jinsi inavyofanya
kazi kwa ufanisi na weledi kwa kuhakikisha inatekeleza mipango yake kwa kasi
inavyotakiwa.
Hatua hiyo inapelekea
utendaji wa kazi za Serikali kuwa bora na zenye tija kwa wananchi siku hadi
siku na zenye nia ya kuleta mabadiliko katika utekelezwaji wa miradi mbalimbali
ambayo hutumia pesa nyingi za umma inayoendana na thamani ya pesa.
Kwa kuzingatia kuwa fedha
zitumikazo katika utekelezaji wa miradi ya Serikali kwa kiasi kikubwa hutumika
kupitia mfumo wa ununuzi wa umma. Ili kuleta tija kwa taifa, Serikali imeamua
kuimarisha eneo hilo kwa kuanzisha Mfumo wa Ununuzi kwa njia ya Kielektroniki
(TANePS) ambao unasimamiwa na Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) chini
ya Wizara ya Fedha na Mipango.
Ili uwe endelevu, mfumo
umetayarishwa kwa mujibu wa Sheria ya Ununuziwa Umma ya Mwaka 2011na Kanuni za
Ununuzi wa Umma chini ya Tangazo la Serikali Na. 446 la Mwaka 2013. Sehemu ya
XI ya Kanuni hizo inabainisha utaratibu wa mfumo wa manunuzi kwa njia ya
mtandao kwa mujibu wa Kanuni ya 343,mambo yatakayotekelezwa kwa mfumo ni pamoja
na usajili wa watumiaji, mchakato wa zabuni, ununuzi wa bidhaa, mnada wa
mtandaoni, malipo ya ada mbalimbali pamoja na usimamizi wa mikataba mbalimbali.
Akizungumza mfumo huo hivi
karibuni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James alisema kuwa mfumo
umeanzishwa ili kuiwezesha Serikali kupata thamani halisi ya fedha zinazotumika
kupitia ununuzi wa bidhaa, huduma na kazi za ujenzi.
Mfumo wa ununuzi umeanza
kutumika tayari kuanzia mwezi Machi 2018 kwa mujibu wa Kanuni ya 342(1) ambapo baadhi
ya taasisi za umma zimeunganishwa baada ya kukamilisha taratibu muhimu ikiwemo
mafunzo kwa watumiaji wa mfumo huo na mfumo huo upo wazi kwa wafanyabiashara
kujisajili.
Akielezea baadhi ya faida
za mfumo huo, Katibu Mkuu James alisema kuwa ni pamoja na kurahisisha ushiriki wa
wazabuni kwenye michakato ya ununuzi na hivyo kuongeza ushindani na ufanisi na
kupunguza muda unaotumika katika mchakato wa zabuni.
“Mfumo huu utaongeza
uwazi na kupunguza vitendo vya rushwa ikiwa ni pamoja na kuongeza kiwango cha uwajibikaji
kutokana na urahisi wa uhakiki wa michakato ya zabuni inayoendeshwa, kupunguza
gharama za ununuzi kutokana na uokoaji wa muda, pamoja na kupunguza
muda wa kuandaa vikao na tathmini yake pamoja na kuimarika kwa utunzaji
wa kumbukumbu za ununuzi.” alisisitiza Katibu Mkuu James.
Inakadiriwa kwamba
kuanzishwa kwa mfumo huu kutaokoa wastani wa shilingi bilioni 34 katika miaka
mitano ya kwanza, hali ambayo itaipunguzia Serikali mzigo mkubwa uliokuwa
unatokana na matumizi yasiyo na tija ambayo yalikuwa kwenye mfumo wa kawaida.
Kwa kuzingatia manufaa ya
mfumo huo, Serikali imeagiza PPRA kuhakikisha kuwa ifikapo tarehe 31, Desemba,
mwaka huu ihakikishe kwamba taasisi zote za nunuzi nchini ziwe zimeungwa katika
mfumo huo.
“ Natoa wito kwa
wazabuni, taasisi binafsi na za umma na
wananchi kwa ujumla kuungana na Serikali kwa kutoa ushirikiano wa kutosha ili
kufanikisha azma ya Serikali ya kuwa na
mfumo wenye tija kwa taifa” alisema James.
Kwa upande wake Afisa
Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Mhandisi Leonard
Kapongo alisema baada ya kupatiwa maelekezo hayo Mamlaka ilianza kutoa mafunzo kuhusiana na matumizi ya mfumo wa
TANePS kwa maafisa wa ununuzi na TEHAMA wa taasisi za Umma.
“Mpaka sasa Mamlaka
imefanikiwa kuunganisha taasisi 418, huku
wataalamu waliopatiwa mafunzo kutoka taasisi nunuzi ikifikia 1,600
ambapo mara baada ya kupatiwa mafunzo taasisi zao huunganishwa kwenye mfumo na
kuendelea kutekeleza michakato yote ya ununuzi inayofuata” alisema Mhandisi
Kapongo.
Mhandisi Kapongo alitoa
rai kwa wakuu wa taasisi kuhakikisha kwamba wanatumia mfumo huo kwani ni takwa
la Sheria ya Ununuzi na Kanuni zake, na kwamba PPRA watafuatilia kwa karibu
kuhakikisha matumizi sahihi ya mfumo huo.
Watoa huduma mbalimbali,
wazabuni na makandarasi wameshauriwa kuchangamkia fursa ya kushiriki kwenye
michakato ya zabuni kwa kujisajili TANePS kupitia tovuti ya mfumo ambayo ni, www.taneps.go.tz ambapo watapata maelekezo
mbalimbali ya namna ya kujisajili.
Akizungumzia faida ya
mfumo huo kwa wazabuni, Mhandisi Kapongo alisema kuwa ni mfumo uliorahisishwa
sana kwa vile hawatahitaji tena kutumia makabrasha au kusafiri kwa ajili ya
kuwasilisha zabuni zao.
“Mambo yote hayo
yatafanyika kwa njia ya mtandao, yakihusisha kutangazwa kwa mipango ya ununuzi
ya mwaka, matangazo mahsusi ya zabuni na Wazabuni waliosajiliwa kuweza kupakua
nyaraka za zabuni na kuziwasilisha kwa taasisi nunuzi kwa njia ya mtandao na
majibu ya washindi wa zabuni yatatangazwa kwenye mtandao wa mfumo” alisema
Mhandisi Kapongo.
Naye Mwenyekiti wa Bodi
ya PPRA, Balozi Dkt, Marten Lumbanga ameunga mkono mfumo huo na kuongeza kuwa utarahisisha
kazi na kuweka uwazi kwa mapato ya Serikali yanayoingia kupitia ununuzi kwa
taasisi za umma.
No comments:
Post a Comment