Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo akizungumza wakati wa mahafali ya
kumi na moja ya Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo kilichopo Jijini Dodoma.
..................................
Nteghenjwa Hosseah OR-TAMISEMI.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI
Mhe. Selemani Jafo amewatunuku wanafunzi 4191 tuzo za Astashahada ya awali,
kati na Stashahada za chuo cha Serikali za Mitaa mapema leo Tarehe
31/10/2019 katika viwanja vya Magufuli Square vilivyopo Hombolo chuoni
hapo.
Akiwa katika Mahafali hiyo Waziri
Jafo amewataka wanafunzi hao kwenda kufanya kazi kwa weledi na uaminifu ili
waweze kutangaza sifa njema ya Chuo cha Serikali za Mitaa.
“Najua wengi hapa mtaajiriwa na
mtaajiriwa katika Halmashauri zetu nataka muende mkazitendee haki halmashauri hizo,
mkafanye kazi kwa bidii na kuleta mabadiliko chanya katika mamlaka zetu za
Serikali za Mitaa”
Chuo hiki kinatoa maarifa stahiki kwa
mahitaji ya soko la ajira la sasa, napokea sifa nyingi za wahitimu wa
chuo hiki wanapofanya kazi katika maeneo mbalimbali nchini, naamini ninyi
mnaohitumu leo mmeiva vyema kwenda kulitumika Taifa hili alisema Jafo.
Aliongeza kuwa Sheria, Taratibu na
Kanuni za Utumishi wa Umma ukawe muongozo wenu katika utendaji kazi wenu wa
kila siku, mkafanye kazi kwa umakini mkubwa ili tuzidi kuwa na wataalamu wenye
weledi ili maendeleo ya Taifa yaweze kufikiwa.
Wakati huo huo Waziri Jafo
amezitaka Halmashauri zote kuanza kutumia mfumo ulioboreshwa wa fursa na
vikwanzo kwa maendeleo ambao umeandaliwa na Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo
kwa kushirikiana na JICA.
“Mfumo huu ulioboreshwa utazisaidia
Halmashauri zetu katika kupambana na vikwanzo vya maendeleo na kuona ni namna
gani zinaweza kutumia fursa zinazopatikana katika maeneo hayo” Alisema Jafo.
Nikipongeze chuo hiki kwa kuwa wabobezi
na mahiri katika maandiko yenye kutoa Dira na muelekeo wa kupambana na
changamoto zilizoko katika Mamlaka za Serikali za Mitaa alimalizia Jafo.
Naye Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Mpamila
Madale amesema chuo hicho mbali na kutoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi
pia wamejikita katika Tafiti, kutoa ushauri wa kitaalam pamoja na kuandaa
machapisho ya kitaaluma.
Alisema mpaka sasa chuo cha Serikali
za Mitaa kina jumla ya wanafunzi 7436 na ongezeko la wanafunzi hao
kumepelekea uhaba wa madarasa ambapo kwa mwaka huu wameweza kujenga darasa moja
lenye uwezo wa kubeba wanafunzi 504 kwa kutumia mapato ya ndani na ujenzi huo
umetumia force account.
Mahafali haya ni mahafali ya kumi na
moja na yamehudhurisha wahitimu wa Astashahada ya awali ya ugavi na manunuzi,
menejiment ya rasilimali watu,utunzaji wa kumbukumbu, pamoja na maendeleo ya
jamii.
Wanafunzi walohitimu kwenye
Astashahada ya kati ni Utawala katika Serikali za Mitaa, Uhasibu na Fedha
katika Serikali za Mitaa, Ugavi na manunuzi,menejiment ya rasilimali watu,
utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka na Astashahada ya kati ya maendeleo ya jamii;
Wakati huo huo wanaofunzi waliohitimu
katika ngazi ya Shahada ni Utawala katika Serikali za Mitaa, Uhasibu na Fedha
katika Serikali za Mitaa, Menejiment ya Rasilimali watu, Maendeleo ya jamii,
Ugavi na manunuzi pamoja na Stashahada ya Utunzaji wa Kumbukumbu 2019.
Mkuu wa chuo cha Serikali za Mitaa Dkt. Mpamila
Madale akiwasilisha hotuba wakati wa mahafali ya kumi na moja ya Chuo cha
Serikali za Mitaa Hombolo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo akiwatunuku wahitimu wa Astashada ya
kati ya ugavi na manunuzi, 2019 ya Chuo cha Serikali za Mitaa – Hombolo
Baadhi ya wanafunzi waliohitimu katika chuo cha
Serikali za Mitaa Hombolo
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na
baadhi ya wanafunzi waliohitimu katika chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo
wakati wa mahafali ya kumi na moja ya chuo hicho kilichopo Jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment