Na
Mwandishi Wetu-Dodoma
Utendaji mzuri katika
eneo lolote ni tunu na uwezo wa kuleta mageuzi ya kweli kwenye jamii yoyote ile
inayolenga kupiga hatua kufikia
maendeleo endelevu yanayotokana na Dira ya Maendeleo iliyowekwa na jamii
husika.
Kufikiwa kwa malengo
hayo katika nchi yetu kunatokana na uongozi madhubuti na utendaji mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwekeza vyema katika Sekta ya Elimu, Nishati,
Maji,Uchukuzi, Mawasiliano na Afya.
Msingi wa Mafanikio
yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka minne yanatokana na aina ya uongozi wa
Rais Magufuli wa kuzingatia kuwapo kwa ushahidi wa mahusiano chanya kati
ya “Kiongozi na Matokeo” sambamba na ukuaji wa uchumi.
Hivyo Basi, uwekezaji
mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika sekta ya elimu umeonesha
mafanikio makubwa kupitia Mpango wa Elimu Msingi (Basic Education) bila malipo wenye lengo la kuhakikisha kuwa kila mtoto
wa Tanzania mwenye sifa ya kwenda shule anapata haki ya kupata elimu bila
kikwazo cha ada na michango mingine.
Katika kukuza sekta hii
Chuo Kikuu cha Sokoine kilipatiwa matrekta 10 mapya ili kufundishia wataalamu
wa kilimo,katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kulifanyika ujenzi wa mabweni,halikadhalika
mikopo kwa wanafunzi wa wa Elimu ya Juu imeongezwa hadi shilingi bilioni 450
kwa mwaka 2019/ 2020 ikilinganishwa na shilingi bilioni 427.5 zilizotengwa
mwaka 2018/2019.
Hatua nyingine ni
pamoja na ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi unaoendelea katika wilaya nyingi hapa
nchini, ujenzi wa madarasa, matundu ya vyoo,maabara na miundombinu mingine ya
sekta hii imechangia kukuza kiwango cha elimu.
Katika sekta ya nishati
Rais Magufuli amewezesha kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa maji katika mto Rufiji unaojulikana kama
mradi wa kufua umeme wa Mwalimu Nyerere
utakaozalisha megawati 2115, hapa Mhe. Rais amewahi kunukuliwa akisema “Umeme
ni Maendeleo, ni kichochea muhimu cha ukuaji wa uchumi kwa taifa lolote,bila ya
kuwepo kwa umeme wa uhakika ndoto yetu ya kujenga uchumi wa viwanda haitatimia.”
Sekta ya uchukuzi nayo
haikuachwa nyuma kupitia utekelezaji wa miradi ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa
kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro umefikia asilimia 70 na kipande cha
Morogoro Makutopora unaendelea kwa kasi na umefikia asilimia 20 , mradi huu
umetoa ajira kwa watanzania wapatao 6,335 sawa na asilimia 90 ya wafanyakazi
wote.
Kukamilika kwa mradi
huu kutachangia kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi kuongezeka na hivyo ustawi wa
wananchi utaleta tija katika uzalishaji.
Uboreshaji wa
miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam mwaka 2018/2019 unaendelea na unalenga
kuifanya kuwa ya kisasa na kuwa na gati zenye uwezo wa kuhudumia meli
nyingi na kubwa zaidi ya ilivyokuwa
awali, kwa sasa gati namba 1 hadi 7 zimeboreshwa na ujenzi wa gati jipya la
kuhudumia meli zilizobeba magari umefikia asilimia 65.
Bandari ya Tanga na
Mtwara nazo zimeboreshwa na kuongeza uwezo wa kuhudumia meli kubwa na kwa idadi
kubwa zaidi, usafiri katika maziwa yote nchini umeimarishwa kwa kujengwa kwa
meli mpya na kukarabatiwa kwa zile zilizopo hivyo wananchi wanaotegemea usafiri
huo katika ziwa Tanganyika, Victoria na Nyasa wameongeza kasi ya shughuli za
kiuchumi.
Baadhi ya Miradi
inayoendelea katika sekta ya uchukuzi ni pamoja na ile ya ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya Ubungo,
upanuzi wa barabara ya Kimara Mwisho hadi Kibaha Km 19.2 kutoka njia mbili hadi
njia nane, ujenzi wa daraja jipya la
Salenda na miundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo kasi Awamu ya II na III.
Kufikia mwezi Februari
2019, jumla ya miradi 65 ya maji vijijini ilikamilishwa ambapo wananchi milioni
25.36 waishio katika vijiji hivyo wamenufaika kwa kupata maji safi na salama,hali
hiyo inaendana na malengo ya Maendeleo
Endelevu ya Umoja wa Mataifa.
Katika kusimamia
rasilimali za nchi Rais Magufuli amewezesha kutungwa kwa sheria kwa ajili ya
usimamizi thabiti wa rasilimali ya madini, Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusu
Umiliki wa Maliasili Na.5 ya mwaka 2017 na Sheria ya Mapitio na Majadiliano
kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi No.6 ya mwaka 2017
pamoja na kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini sura ya 123.
Kwa upande wa Sekta ya Kilimo
inayoajiri wananchi takribani asilimia 75 hadi 80 ambapo kwa kutambua umuhimu
wa sekta hii Rais Magufuli alizindua Programu ya kuendeleza Sekta ya Kilimo
Awamu ya Pili (ASDP II). Programu hii inalenga kuleta mageuzi katika sekta hii
kwa maana ya mazao, mifugo na uvuvi ili kuongeza uzalishaji na tija,
kufanya kilimo kiwe cha kibiashara na
kuongeza pato la wakulima hususan wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha maisha
na usalama wa chakula na lishe.
Kwa kuwa Rais Dkt.
Magufuli amewezesha ujenzi wa vituo vya afya 352 na hospitali za wilaya 67 na hospitali
za kanda zinaendelea kujenga ni wazi kuwa mchango wake katika kuboresha maisha
ya wananchi unamfanya kuwa na sifa za
kutunukiwa shahada hii. Hakika usemi wa wahenga usemao chanda chema huvikwa
pete leo umetimia kwa Mhe. Rais Magufuli kutunukiwa Shahada ya Sayansi ya
Udaktari wa Falsafa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment