Sunday, November 3, 2019

NECTA yaonya wadanganyifu wa mitihani, Kundi la kwanza elimu bure kufanya mitihani kesho




BARAZA la mitihani Tanzania (NECTA) limetangaza kuanza kwa mitihani ya kidado cha nne kwa mwaka 2019 hapo kesho huku ikisisitiza kuwa wamechukua hatua zote muhimu kuhakikisha vitendo vya udanganyifu vinadhibitiwa.

Idadi ya wanafunzi ambao wamejiandikisha kufanya mtihani huo imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka na kwa mwaka huu jumla ya watahiniwa 585,866 wamesajiliwa kufanya mtihani huo. Kati yao watahiniwa wa shule ni 433,052 na watahiniwa wa kujitegemea ni 52,814

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dkt Charles Msonde amesema vitendo vya udanganyifu katika mitihani imeendelea kushuka mwaka hadi mwaka na mwaka huu wamejipanga kuvidhibiti.

Akitoa Takwimu ya kupungua kwa vitendo hivyo, Dkt Msonde alisema, toka Mwaka 2011 ambapo vitendo hivyo vilikuwa vikubwa na kupelekea kufuta matokeo, vitendo hivyo vilianza kushuka.

Alisema mwaka 2011, upande wa elimu ya msingi Barazalilirekodi vitendo vya udanganyifu 9,736 na baada ya hapo viliendelea kupungua mwaka hadi mwaka na ilipofika mwaka 2018 vitendo hivyo vilifikia 200+.

Kwa upande wa sekondari pia vitendo hivyo kwa mwaka 2011 baraza lilirekodi jumla ya vietendo vya udanganyifu 3303, idadi iliendelea kupungua hadi kufikia 200+ mwaka jana

“Napenda kuchukua nafasi hii kuzipongeza kamati zetu za mikoa, halmashauri kwa juhudi ambazo wanazichukua kukabiliana na udanganyifu wa mitihani, kwa kweli tumevipunguza sana na mwelekeo wetu ndio huo, kukabiliana na vitendo hivyo.” Alisema Dkt Msonde

Aidha Msonde aliongeza kuwa kufuatia mafanikio hayo, jumla ya Nchi 10 za SADC ziliweza kuja Tanzania kujifunza namna Taasisi hiyo ilivyoweza kukomesha udanganyifu.

Kuhusu watahiniwa wenye mahitaji maalum, Dkt Msonde alisema kwa mwaka huu kuna Jumla ya wanafunzi 842 ambao kati yao 450 ni wenye uoni hafifu, 42 wasion kabisa, 200 wwenye ulemavu wa kusikia na 150 wenye ulemavu wa viungo vya mwili.

Ametoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa, halmashauri,Manispaa, Jiji kuhakikisha kuwa taratibu zote za mitihani ya Taifa zinazingatiwa ipasavyo, pia amewataka wasimamizi wote wa mitihani kufanya kazi yao kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu.

Aidha watahiniwa wote wenye mahitaji maalum, wasimamizi wanatakiwa kulinda haki zao ikiwamo kuwapa mitihani yenye maandishi makubwa kwa wale wenye uono hafifu na mitihani yenye maandishi ya nukta nundu kwa watahiniwa wasioona.

Na wale wenye mahitaji maalum waongeze muda wa dakika 20 kwa kila saa kwa somo la hisababti na dakika 10 kwa kila saa kwa masomo mengine kama mwongozo wa baraza unavyoelekeza.

Hilo ni kundi la kwanza la wanafunzi wa kidato cha nne walionufaika na mpango wa elimu bila malipo

Kwa upande wake Waziri wa Tamisemi Suleiman Jaffo amesema hiyo ni hatua kubwa kwa serikali ambayo inatekeleza mpango huo ambao umesaidia kuongeza idadi ya wanafunzi walioendelea na sekondari.

Waziri Jafo amewataka watahiniwa kujiepusha na vitendo vya udanganyifu na kuhakikisha wanadumisha amani na utulivu wakati wote wa mitihani.

 “Hili ni jambo kubwa kwa kuwa hawa  ni watahiniwa wa kwanza walianza shule mwaka 2016 tuna kila sababu ya kumshukuru Rais Magufuli kwa utashi wake wa kisiasa na kuja na mpango huu.”

 “Niwaombe wanafunzi na wote wanaohusika katika usimamizi wa mitihani wajiepushe na vitendo vya udanganyifu, najua baraza la mitihani haliwezi kuvumilia na msije kulilaumu kwa kuonyesha makali yake,” amesema Jafo.

No comments:

Post a Comment