Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Dodoma
Michezo
ni nyenzo madhubuti katika kulinda afya za wanadamu kwa kuwajengea uimara na
ustahimilivu, kukuza stadi za kijamii kiubunifu na kiuongozi ili kuwawezesha
wanamichezo na watu wote kujifunza vitu vipya vinavyoweza kuchangia kutunza
afya zao ili waweze kujiletea maendeleo yao wenyewe na taifa kwa ujumla.
Sera
ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995 inatambua umuhimu wa michezo ikiwemo kuhamasisha
Umma wa Watanzania kushiriki katika michezo na mazoezi ya viungo. Kwa kutambua
jambo hilo, Serikali imewezesha upatikanaji wa viwanja na vifaa vya michezo
vilivyo bora na vya kutosha kwa ajili ya kuimarisha maendeleo ya michezo
nchini.
Kama
taifa, kumekuwa na mtazamo chanya kwa viongozi kuthamini michezo kuanzia ngazi
ya Serikali Kuu hadi Serikali za Mitaa kupitia mikoa, wilaya, tarafa, kata,
vijiji, mitaa na vitongoji.
Kwa
kulitambua na kulithamini suala la michezo kwa watu wa rika zote kuwa ni muhimu
kwa afya, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan mwaka 2016 alipokuwa akizindua kampeni ya kitaifa ya kudhibiti magonjwa
yasiyo ya kuambukiza kwenye viwanja wa Leaders Club jijini Dar es Salaam aliagiza
watu katika maeneo yao nchini kushiriki kufanya mazoezi ambayo ni sehemu ya
michezo.
Ili
utaratibu wa kufanya mazoezi uwe endelevu, Makamu wa Rais alisisitiza “……….kila
Jumamosi ya pili ya mwezi itakuwa siku ya mazoezi kwa afya, kwa sababu mazoezi
ni afya na nawaasa wananchi kufanya mazoezi na kuanzisha na kujiunga na vikundi
vya mazoezi na Serikali itatimiza wajibu wake wa kuweka mazingira mazuri ya
kufanyia mazoezi kote nchini.”
Wananchi
wamekuwa na mwitikio mkubwa katika kulifanyia kazi agizo hilo kwa kuweka utaratibu
wa kufanya mazoezi ambao umeongeza idadi ya vikundi vya mazoezi ya pamoja
katika maeneo mbalimbali ya nchini.
Hamasa
ya kufanya mazoezi sasa imekuwa nzuri ambapo Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto zimeanzisha utaratibu wa kuwa na bonanza, matamasha ya michezo
pamoja na vilabu vya kufanya mazoezi. Hatua hii imekuwa ni chachu mpya ya kutekeleza
agizo la Makamu wa Rais Mama Samia la kufanya mazoezi kwa manufaa ya afya za
Watanzania.
Akiwasilisha
Bungeni hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2019/2020
ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Waziri mwenye dhamana ya
wizara hiyo Dkt. Harrison Mwakyembe aliliambia bunge na Watanzania wote kuwa,
miongoni mwa majukumu ya sekta ya michezo ni kuratibu na kusimamia maendeleo ya
michezo nchini ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika
michezo.
Mojawapo
ya vitu vinavyoshirikisha watu wengi kujiunga na kufanya mazoezi ni kuwa na
matamasha ya michezo mbalimbali ambayo yanalenga kuhamasisha wananchi kushiriki
katika michezo ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi ya viungo ili kukabiliana na
magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi hapa nchini.
Magonjwa
hayo hutokana na mitindo isiyofaa ya maisha kama matumizi ya tumbaku, lishe
duni, matumizi ya pombe kupita kiasi, pamoja na kutoshughulisha mwili au
kutofanya mazoezi ya viungo mara kwa mara. Magonjwa kama kisukari, shinikizo la
juu la damu, magonjwa ya moyo na mishipa, saratani, pumu na magonjwa ya akilini
miongoni mwa magonjwa hayo, ambapo yasipodhibitiwa huwa na sugu na yenye
kuhitaji gharama kubwa kuyatibu.
Hapo
awali, magonjwa hayo yalikuwa yakiwaathiri watu wenye umri mkubwa zaidi ya
miaka 45, lakini kwa sasa yanazidi kuathiri watu watu wengi wakiwemo watoto wenye
umri mdogo.
Naibu
Wiziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza hivi karibuni
akiwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa tamasha la michezo la wiki ya kuzuia na
kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza lililofanyika Novemba 09, 2019 katika uwanja
wa Jamhuri Dodoma alihimiza watu kuchukua uamuzi wa kufanya mazoezi ili kujenga
afya zao.
“Mazoezi
ni jambo lolote linalohusisha misuli na kusababisha kuongezeka kwa mapigo ya
moyo na kasi ya kupumua. Wataalam wa afya wanasema kuwa kiwango cha mazoezi kinacholeta
faida ni mazoezi yasiyopungua dakika 30 kwa siku angalau siku tatu kwa wiki na
yanayomfanya mtu kutokwa na jasho” alisisitiza Naibu Waziri Shonza.
Kwa
mujibu wa Naibu Waziri Shonza watumishi wanaofanya kazi ofisini wametakiwa kuongeza
bidii ya kufanya mazoezi kulingana na mtindo wa maisha ya mtumishi mmoja mmoja
kuendana na hali yake ya maisha.
Kwa
watumishi wa umma na sekta binafsi pamoja na watu wengine wanaotumia magari, wanapaswa
kupanga shughuli ambazo zitawafanya kila siku watembee kwa miguu, wanaoishi au
kufanya kazi ghorofani wajitahidi na wajizoeshe kutumia ngazi kila siku badala
ya lifti, mtu anapokwenda mahali popote watumie njia ndefu kutembea badala ya
njia ya mkato pamoja na kupunguza muda wa kutazama televisheni, badala yake muda
huo utumike kufanya shughuli zinazotumia viungo vya mwili kama kufua, kuosha
vyombo, kuosha gari, kusafisha nyumba, kazi za bustani na kufyeka majani ambazo
zinasaidia kujenga utimamu wa mwili.
Naibu Waziri Shonza ametoa rai kwa waajiri kuboresha mazingira ya kazi kwa
kuhakikisha watumishi wao wanashiriki katika michezo na kufanya mazoezi hata
maeneo yao ya kazi na kutoa mfano wa
kuanzisha timu mbalimbali za michezo na kutenga siku maalum katika mwezi kwa
ajili ya mabonanza ya michezo. Mazingira rafiki ya kufanyia mazoezi kazini ni
pamoja kutenga vyumba vya mazoezi na na kununua vifaa vya michezo. Hatua hiyo itaimarisha
afya za watumishi na kupunguza gharama za matibabu katika taasisi husika.
Aliongeza
kuwa ili kufanya mazoezi kuwa endelevu, maafisa michezo na utamaduni wa mikoa
na wilaya wana wajibu wa kuongeza uhamasishaji na uundaji wa vikundi vya
mazoezi ya pamoja katika maeneo yao.
Wizara
nyingine zenye uhusisano na mchango katika kufananikisha wananchi kufanya
mazoezi ni Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Wizara hizo zina mamlaka
ya kusimamia na kuweka mazingira bora ya watu kufanya mazoezi kwa kuendelea
kutenga viwanja vya michezo na kuzuia uuzaji wa maeneo ya wazi hususani viwanja
vya michezo na kuboresha barabara za waenda kwa miguu na baiskeli ili
kuhamasisha watu kutembea na kuongeza usalama wa mazoezi.
Aidha,
mamlaka za usafiri, zinawajibu wa kuboresha usafiri wa
jumuiya ili kuongeza idadi ya watu wanaotumia usafiri wa jumuiya kwa sababu
tafiti nyingi zinaonesha kuwa utumiaji wa usafiri wa jumuiya unaongeza
uwezekano wa kutembea na kufanya mazoezi na hivyo kupunguza magonjwa
yasiyoambukiza.
Matamasha
ya michezo pamoja na matamasha mengine yakiwemo ya utamaduni yanatakiwa kuwa kichocheo
cha kushirikisha vitu vingi ikiwemo michezo ya jadi na mashindano ya baiskeli
katika maeneo mbalimbali ambayo yana mchango mkubwa katika kutunza afya za
washiriki wa michezo hiyo.
Wakati
wa matamasha hayo, ni vema wananchi wahamasishwe kupima afya zao hususani wa magonjwa
yasiyoambukiza kwani tiba ya mapema ina manufaa kwa kuwa inapunguza uwezekano
wa watu kupatwa na madhara zaidi. Hatua hiyo inaweza kuondoa magonjwa hayo moja
kwa moja. Ili kuongeza hamasa ya wananchi na wanamichezo kupima afya zao,
upimaji huo unapaswa kuwa ni wa bure ili watu wengi zaidi wapate fursa ya kupimwa.
Hivi
karibuni Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa mwongozo wa kudhibiti magonjwa
yasiyo ya kuambukiza ambapo mataifa yameazimia kutekeleza malengo ya maendeleo
endelevu, (SDGs) ili kupunguza kwa theluthi moja vifo vya mapema vitokanavyo na
magonjwa yasiyo ya kuambukiza ifikapo mwaka 2030.
Akizungumzia
mwongozo huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Tedros
Adhanon Ghebreyesus alisema, “Zaidi ya nusu ya watu duniani wanaishi mijini, na
idadi yao inaongezeka. Viongozi wa miji wanapaswa kuchukua maamuzi ambayo yataboresha
afya za wakazi wao, ili miji iweze kuchipua na kustawi. Kila mtu anapaswa
kupata huduma ambazo zitaboresha afya, huduma za usafiri wa umma ziwe salama,
makazi ya nje yawe safi na salama, mlo uwezo mzuri na huduma za afya ziwe
bora.”
Naye
Balozi wa WHO katika kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs) na
majeraha, Michael Bloomberg alisema kuwa shirika hilo lipo mstari wa mbele
katika kusambaza mikakati hiyo duniani kote ili kuokoa maisha ya mamilioni ya
watu.
“Tunafanya
kazi kuhamasisha uelewa miongoni mwa viongozi wa miji na watunga sera kuhusu
manufaa halisi yanayoweza kupatikana pindi programu hii ya kuboresha miji
inapofanya kazi.” alisisitiza Balozi Bloomberg.
Ni
kweli, wataalamu wa afya wanashauri kuwa ni vema kila mtu awajibike kuitunza
afya yake kwa kufuata mtindo bora wa maisha kwani afya njema ni msingi wa
maendeleo. Hatua hii inaunga mkono kauli mbiu tamasha la michezo la wiki ya
kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyo ambukiza inayosema “Tutembee pamoja katika kuzuia
na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza.”
No comments:
Post a Comment