Wednesday, November 13, 2019

WATOA HUDUMA WATAKIWA KUJIEPUSHA NA RUSHWA

  Afisa Mwandamizi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bi. Heavenlight Majule akiwasilisha mada kuhusu udhibiti wa
rushwa mahala pa kazi.
............................................


Watoa huduma wa afya wameaswa kuzingatia uadilifu na uaminifu mahala pa kazi kwa kutokuomba wala kupokea rushwa wakati wa kutoa huduma.

Hayo yamezungumzwa na Afisa Mwandamizi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakati wa kufunga mafunzo elekezi kwa
wataalam tarajali 80 walioko kwenye mafunzo ya mwaka mmoja katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa njia ya vitendo yanayolenga kuwawezesha kutoa huduma bora za afya kwa jamii.


“Kupokea zawadi au pesa kabla na baada ya kutoa huduma ni kosa kisheria na pindi utakapogundulika umefanya hivyo basi utachukuliwa hatua kulingana na

vifungu 24 vya makosa ya rushwa vilivyoainishwa katika sheria namba 11 ya mwaka 2007 ya kuzuia na kupambana na rushwa,” Amesema Bi. Majule.

Amesisitiza kila mmoja ana wajibu wakushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa huduma bora za afya bila malipo yoyote kwani rushwa humnyima haki anayepatiwa huduma na kupunguza ufanisi katika kazi.


Kwa upande wake Muuguzi katika Hospitali ya Mloganzila, Bw. Mosama John ametoa wito kwa wataalam hao kuwa na kauli nzuri wakati wa kuwahudumia wateja wanaokuja hospitalini hapa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.


Mada ziliwasilishwa katika mafunzo hayo ni pamoja na elimu elekezi juu ya udhibiti wa rushwa mahala pa kazi, elimu ya maambukizi ya ukimwi na jinsi ya kujikinga, kanuni za maadili ya utendaji kwa watumishi wa Umma, matumizi bora ya vifaa tiba na dawa, huduma za kliniki, mahusiano kwa Umma na huduma kwa wateja.

No comments:

Post a Comment