JUMLA ya watumishi wa umma 2,059 wamekwisharipoti Dodoma katika awamu ya
kwanza ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe
Magufuli aliyoitoa wakati akikabidhiwa uenyekiti wa CCM, Julai 22, mwaka jana.
Awamu ya kwanza ya Serikali kuhamia Makao Makuu Dodoma inajumuisha
Mawaziri na Manaibu wao, Makatibu Wakuu na manaibu wao, baadhi ya wakurugenzi
pamoja na wasaidizi wachache.
Hayo yamebainika leo (Ijumaa, Machi 3, 2017) katika Kikao cha Kazi cha
Mawaziri na Naibu Mawaziri kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Hazina
mjini Dodoma chini ya uwenyekiti wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Katika mkutano huo, Waziri Mkuu aliwataka Mawaziri wote watoe taarifa za
idadi ya watumishi wao waliohamia Dodoma hadi sasa, wamepanga kufanya zoezi
hilo kwa awamu ngapi na lini watakamilisha zoezi hilo. Pia Mawaziri hao
walitakiwa kueleza mahali zilipo ofisi zao kwani amepanga kuwatembelea na
kuzungumza na watumishi.
Wakiwasilisha taarifa hizo, Mawaziri hao wote wamethibitisha kwamba
tayari ofisi zao na wao wenyewe wameshahamia Makao Makuu Dodoma pamoja na
watumishi wao wote walioko kwenye awamu ya kwanza na wameahidi kukamilisha
kuhamisha waliosalia katika awamu nne hadi sita kulingana na ratiba ya
Serikali.
Aidha, Waziri Mkuu amesema baada ya Serikali kukamilisha ratiba ya
kuhamia Makao Makuu Dodoma, Jiji la Dar es Salaam litabakia kuwa Jiji la
kibiashara na wamepanga kuendelea kuendelea kuliboresha ili shughuli hizo
zifanyike kwa ufanisi zaidi.
Mapema, akizungumza na waandishi wa habari wakati akifungua kikao
hicho, Waziri Mkuu alisema kati ya Julai 2016 na Januari 2017, Tume ya
Kudhibiti Dawa za Kulevya iliwakamata watu 11,303 ambao wanatuhumiwa
kujihusisha na uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya.
Alisema kati ya hao, watu 9,811, walikutwa na kesi za kujibu ambapo 9,174
wametiwa hatiani, 238 hawakukutwa na hatia na wengine 478 upelelezi wa kesi zao
unaendelea. Pia alisema tangu Tume mpya iundwe Februari mwaka huu, jumla ya
watuhumiwa 79 wametiwa mbaroni na uchunguzi wa kesi zao unaendelea.
“Wengi kati ya hao, wameshikwa na vithibitisho, ingawa uchunguzi wa kesi
zao bado unaendelea. Na hawa ni wale waliokamatwa na dawa za viwandani kama heroine na cocaine.
Hatujawaingiza wale waliokamatwa na mirungi au bangi. Bado mikoa inaendelea na
kazi, na hii operesheni ni ya nchi nzima,” alisema.
Uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) ambao chimbuko lake ni agizo lililotolewa Oktoba Mosi, 1973
kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa chama cha TANU.
Tangu wakati huo Serikali zote ziliendelea kufanya juhudi
mbalimbali za kuandaa miundombinu na hata awamu ya nne ilisimamia kwa kiwango
kikubwa uwekaji wa miundombinu hiyo.
Serikali ya awamu ya tano iliamua kuhamia Dodoma baada ya kuridhishwa na
ujenzi wa miundombinu na maeneo ya kutolea huduma za kijamii kwa wageni na
wenyeji.
No comments:
Post a Comment